The House of Favourite Newspapers

Wanafunzi waaswa kwenda sambamba na teknolojia

0

Mgeni rasmi katika mahafali ya 13 ya kidato cha nne katika shule ya sekondari Shimbwe iliyopo Uru wilayani Moshi vijijini,Ofisa Mkuu wa Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania,Georgia Mutagahywa akitoa hotuba yake katika mahafali hayo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki shuleni hapo.

Mgeni rasmi katika mahafali ya 13 ya kidato cha nne katika shule ya sekondari Shimbwe iliyopo Uru wilayani Moshi vijijini,Ofisa Mkuu wa Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania,Georgia Mutagahywa(watatu toka kulia) akimtunuku cheti Loth Rajabu ambaye ni mmoja wa wahitimu katika shule hiyo.

Mwanafunzi wa kidato cha Nne Christina Lyimo(kushoto) wa Shule ya Sekondari Shimbwe iliyopo Uru wilayani Moshi vijijini,akitunukiwa cheti na mgeni rasmi katika mahafali ya 13 katika shule hiyo, Ofisa Mkuu wa Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania,Georgia Mutagahywa mwishoni mwa wiki.Balozi Mwanaidi Majaar(kulia) akijadiliana jambo na mgeni rasmi wa mahafali ya 13 ya shule ya sekondari Shimbwe iliyopo Moshi vijijini, Ofisa Mkuu wa Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania,Georgia Mutagahywa (kushoto) mara baada ya kutembelea chumba cha mafunzo ya Kompyuta katika shule hiyo.

Mgeni rasmi wa mahafali ya 13 ya shule ya sekondari Shimbwe iliyopo Moshi vijijini, Ofisa Mkuu wa Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania,Georgia Mutagahywa (kushoto ) akiongozana na mkuu wa shule ya sekondari hiyo ,Jacob Costantine kuelekea katika jukwaa wakati wa mahafali hiyo ya kidato cha nne katika shule hiyo.

Wanafunzi wanaokwenda sambamba na teknalojia wanayo nafasi kubwa zaidi ya kufanya vizuri kwenye masomo yao endapo wataitumia kwa mtizamo chanya.Kwa mtizamo huo, wanafunzi wametakiwa kutokubali kubaki nyuma kiteknalojia haswa katika karne hii ya 21 ambayo ni karne ya sayansi na teknalojia.

Hayo yalibainishwa na Bi Georgia Mutagahywa, Ofisa Mkuu wa Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, ambaye alikuwa mgeni rasmi wa mahafali ya 13 ya kidato cha Nne katika shule ya Shimbwe iliyopo Uru Moshi vijijini aliyekuwa ameongozana na Mwenyekiti wa Hassan Majaar Trust (HMT) Balozi Mwanaidi Majaar alisema kampuni ya Vodacom Tanzania inatarajia kuleta wataalamu kutoka Learning In Sync kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa walimu na wanafunzi wa shule hiyo.

“Teknolojia ndiyo mkombozi na ndiyo sababu sisi tunasema hakuna mtoto atakayebaki nyuma katika teknolojia. Siku za usoni watakuja wataalamu ambao ni wadau wetu wakubwa katika masuala ya teknolojia ambao wataweza ku train(toa mafunzo) waalimu na wanafunzi katika programu mbalimbali kwa kutumia silabasi za kitanzania.”alisema Mutagahywa.

Pia aliendelea kusema kuwa kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania kupitia mfuko wake wa kusaidia jamii”Vodacom Foundation” imepanga kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la T-MARC Tanzania kutoa mafunzo kwa wanafunzi wa shule ya sekondari ya Shimbwe juu ya kubadili maisha ya watoto ,kimalezi na kimakuzi.

Hatua ya Vodacom foundation kuchukua jukumu hilo inatokana na taarifa ya baadhi ya watoto wa kike katika shule hiyo kushindwa kumaliza masomo yao ya sekondari kutokana na kubeba ujauzito wakiwa shuleni.Akiendelea kuzungumza katika mahafali hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki ,Georgia alisema Vodacom kwa kutambua changamoto hiyo imepanga kutoa nyenzo kwa watoto wa kike.

“Hili suala la Mimba za utotoni tuna wadau wanaofanya kazi na watoto wa kike na tunatambua changamoto za mtoto wa kike,lakini tunataka kuwapa nyenzo za kuwawezesha kuvuka na mnaweza kuvuka na mkawa wanawake wa maana katika uongozi wa nchi”alisema Mutagahywa.

“Ni lazima tufike mahali ambapo watoto wetu wa kike na kiume tuone wanaweza kuheshimiana na kusaidiana ili taifa liweze kusonga mbele …Hata ukipata mimba ukisha jifungua rudi shule ukasome,ukianguka unanyanyuka na unaendelea…..kwa hiyo nitazungumza na wadau wetu T-MARC waje wazungumze na wasichana na wavulana kuhusu suala la mimba kwa sababu si mimba zote zinatoka kwa fataki.”aliongeza Mutagahywa.

Kwa upande wake Balozi Majaar alitoa pongezi kwa kampuni hiyo na wanafunzi wa kidato cha Nne na kuwatakia kila la heri katika mitiani yao ijayo na pia alimpongeza Ofisa huyo wa Vodacom Tanzania kwa kuendelea kusaidia jamii ya watanzania hasa katika eneo la Elimu ambalo limekuwa likikabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za madawati.

“Niwashukuru sana Vodacom Tanzania,hasa mgeni rasmi ni mwanamke ambaye yeye muombe chochote hasa kwenye masuala ya elimu ,atajitolea na wakati mwingine huchangisha wafanyakazi wenzake ili pesa zipatikane kuchangia shule,tulivyomuomba hakusita kwa vile tayari aliwahi kuja shimbwe kuangalia juu ya masuala ya kompyuta”alisema Balozi Majaar.

Awali akisoma taarifa mbele ya mgeni rasmi mkuu wa shule ya sekondari Shimbwe,Jakob Costantine alisema shule yake inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya nyumba za walimu hali inayowalazimu kuishi mbali na ilipo shule hiyo.

“Ombi letu kwa serikali itusaidie upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ukarabati mkubwa wa majengo ya shule na nyumba za walimu na upatikanaji wa tanki kubwa kwa ajili ya kuhifadhia chakula”alisema Costantine.Mbali na Ombi hilo ,Mkuu huyo wa shule aliomba kujengwa wa mnara kwa ajili ya mawasiliano ya simu katika maeneo ya jirani na shule ili kuwezesha upatikanaji wa urahisi wa mawasiliano pamoja na kurahisisha mafunzo ya kompyuta shuleni hapo.

Leave A Reply