Wanafunzi Walivalia Njuga Sakata la Mimba za Utotoni

WANAFUNZI wa shule za sekondari Wilaya ya Busega Mkoa wa Simiyu wameziomba bodi, na uongozi wa shule kuwa na kikao cha pamoja ili kujadili suala la mimba za utotoni.

 

 

Ushauri huo umetolewa baada ya kongamano lililoandaliwa na Diwani wa Kata ya Nyashimo, Mickness Mahela, ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya maendeleo ndani ya kata hiyo.

 

 

“Kuwepo kwa mijadala ya mara kwa mara kupitia kwenye uongozi wa shule,bodi pamoja na wazazi katika shule husika inaweza kusaidia kuepukana na mimba za utotoni,” amesema Annastazia Machumu mwanafunzi wa Shule ya Nasa.

 

Aidha Kabula Mrisho mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Bulingwa ameishauri Serikali kutoa elimu ya kijinsia pamoja na kundi-rika mashuleni ili kuzuia mimba za utotoni.

 

 

Kwa upande wake Mahela amesema kongamano hilo litakuwa la kuzungumza na wanafunzi ili kupunguza changamoto zinazopelekea kupata mimba za utotoni.

 


“Baada ya kongamano hilo tunahitaji kuzungumza na wazazi ili wazazi watambue majukumu yao kwa sababu ili ufaulu mzuri uwepo lazima vitu vitatu vishirikiane ambavyo ni wazazi, mwalimu na serikali ingawa mwalimu ni kiunganishi lakini walezi wakubwa wa watoto ni wazazi,“ amesema Mahela.

 

 

Amesema wamejipanga kuhakikisha kuwa wanafaulisha watoto wengi kama walivyofanya mwaka jana na kwamba watahamasisha madiwani wa kata zingine ili kuifanya ajenda yao iwe ya kupunguza tatizo la mimba za utotoni.

NA OSCAR MIHAYO, BUSEGA

Toa comment