Wanafunzi Watatu wa Shahada ya Uzamili ya Kiswahili UDSM Wafadhiliwa na Alaf

Jumatano 18 Desemba 2024: Katika azma yake kuunga juhudi za serikali katika kukuza Kiswahili, Kampuni ya ALAF Limited leo imetoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi watatu wanaofanya Programu ya Shahada ya Uzamili ya lugha ya kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Akizungumza wakati akikabidhi hundi kwa wanufaika hao watatu, Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa ALAF, Bi.Hawa Bayumi alisema hatua hiyo imelenga kuunga mkono juhudi za serikali za kukuza lugha ya kiswahili ndani na nje ya nchi.
“Kiswahili ni moja ya tunu kubwa tuliyorithi kutoka kwa Muasisi wa Taifa letu la Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, hivyo sisi kama wadau wa maendeleo, tumeona hatuna budi kuunga mkono juhudi za serikali katika kuikuza lugha hii adhimu”, alisema.

Aliendelea kusema kuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimekuwa na jukumu kubwa na muhimu katika kuandaa na kutekeleza Tuzo ya Kiswahili ya Safal ya Fasihi ya Afrika, ambazo ALAF inadhamini pamoja na makampuni yake tanzu yaliyopo nchini Kenya na Uganda na ambayo inawaunganisha waandishi kutoka ukanda wa Afrika Mashariki.
“Sisi kama moja wapo ya makampuni yaliyopata mafanikio makubwa tumeona umuhimu wa kukuza kiswahili na ndiyo maana tutaendelea kuunga mkono juhudi zote zinazolenga kuikuza lugha hii”, alisema.
Aliwataja wanufaika wa ufadhili huo wa ALAF Limited, kuwa ni pamoja na Bi.Asha Ally Mustapha ambaye atapata ufadhili wenye thamani ya Tsh 3,900,000, Bi. Asia Omary Saidi-3,900,000 na Bwana. Fredrick Venance -3,900,000, ambapo jumla ya ufadhili huo ni Tsh 11, 700,000.
Kadhalika, Alitoa wito kwa wanufaika kutumia ufadhili walioupata vyema kwa kuhakikisha wanafanya vyema kwenye masomo yao ili waweze kutoa mchango mkubwa katika kuikuza lugha adhimu ya kiswahili kupitia elimu watakayoipata.
Kwa upande wa Uongozi wa chuo kikuu cha Dar es Salaam umeishukuru kampuni ya ALAF Limited kwa ufadhili huo, ambao umesema kuwa ni sehemu ya maombi mengi yaliyofanywa na wanafunzi wengi.
“Kwa kawaida huwa kuna maombi mengi kutoka kwa wanafunzi kuhusiana na ufadhili huu lakini ni wanafunzi watatu pekee ndio wanaonufaika; kwa hili tunawashukuru sana ila tunaomba mfikirie jinsi ya kuongeza idadi ya wanufaika ili lugha ya kiswahili iweze kukua zaidi”, alisema Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Prof. Rose Upor.
ALAF Limited ni kampuni inayoongoza nchini Tanzania katika kutoa suluhisho mbalimbali za ujenzi ikiwemo kutengeneza bidhaa za uezekaji kwenye majengo iliyoanzishwa mwaka 1960 na tangu wakati huo imekuwa kinara katika kutengeneza bidhaa za uezekaji pamoja na bidhaa zingine za chuma ukanda wa Afrika Mashariki.
Mbali na bidhaa za uezekaji ALAF Limited pia ni kinara katika kutengeza bidhaa zingine kama vile koili za chuma na mabomba ya chuma kwa ajili ya matumizi mbalimbali jambo ambalo linaifanya kampuni hiyo kuwa kinara katika sekta ya ujenzi ukanda wa Afrika Mashariki.