The House of Favourite Newspapers

Wanahisa Wa DCB Wapata Gawio

0
Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Biashara ya DCB, Prof. Lucian Msambichaka (wa pili kulia),  akizungumza na wanahisa wakati wa Mkutano Mkuu wa 18 wa Wanahisa wa benki hiyo ulifanyika kwa njia ya mtandao  jijini Dar es Salaam jana. Wengine kutoka kushoto ni; Mwanasheria wa Makampuni, Alex Mgongolwa, Mkurugenzi wa Sheria na Katibu wa Kampuni, Regina Mduma, Mkurugenzi Mtendaji, Godfrey Ndalahwa na Mjumbe wa Bodi ya benki hiyo, Zawadia Nanyaro.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya DCB, Godfrey Ndalahwa akizungumza na wanahisa  wakati wa Mkutano Mkuu wa 18 wa Wanahisa wa benki hiyo.
Kaimu Mkurugenzi wa fedha wa Benki ya Biashara ya DCB, Ester Bgoya akitoa taarifa za kiutendaji wa kifedha kwa wanahisa wakati wa Mkutano Mkuu wa 18 wa Wanahisa wa benki hiyo.
Mkurugenzi wa Sheria wa DCB na Katibu wa Kampuni, Regina Mduma akizungumza  na wanahisa wa benki hiyo kwa njia ya mtandao katika Mkutano Mkuu wa 18 wa Wanahisa wa benki hiyo.
Mjumbe wa Bodi ya Benki ya Biashara ya DCB, Zawadia Nanyaro akichangia hoja katika mkutano mkuu wa 18 wa wanahisa wa benki hiyo ulifanyika kwa njia ya mtandao ofisini mwa benki hiyo jijini Dar es Salaam.

 

WANAHISA wa BENKI ya Biashara ya DCB wana kila sababu ya kuwa na matumaini na benki yao baada ya Bodi ya benki hiyo kutangaza gawio la shs 5.40 kwa kila hisa wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wanahisa wa DCB uliofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

 

Akitangaza gawio hilo lililopitishwa na wanahisa wote kwa njia ya mtandao, Mwenyekiti wa Bodi anayemaliza muda wake wa DCB. Prof. Lucian Msambichaka alisema gawio hilo limetokana na faida waliyopata ya shs bilioni 2.038 baada ya kodi kufikia Disemba 31, 2019 huku kiasi cha shs milioni 500 kikitumika kulipia gawio hilo.

 

 

Akizungumza zaidi mwenyekiti huyo alisema bodi ilifikia azma ya kulipa gawio la kiasi hicho licha ya faida waliyopata kwa kuzingatia sababu mbalimbali ikiwemo hali ya kibiashara iliyopo nchini iliyochangiwa kwa kiasi kikubwa na athari za ugonjwa wa homa kali ya mapafu wa Covid-19.

 

 

“Sababu nyingine muhimu iliyochangia azma ya kutoa gawio hili ni kutumia faida hiyo kuiwezesha benki kuendelea kuimarisha mtaji hivyo kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi na kupata faida.

 

“Mafanikio ya DCB yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na mchango mkubwa unaotoka kwa wanahisa wa benki yetu kwani hata mwaka 2018 pale benki yetu ilipopata faida ya shs milioni 995, bado wanahisa wetu waliazimia kutumia faida hiyo kuimarisha mtaji badala ya kugawana faida,” aliongeza Prof. Msambichaka.

 

 

Akizungumza na wanahisa hao Mkurugenzi Mtendaji wa DCB, Godfrey Ndalahwa alisema benki imeendelea kuimarika kimtaji huku wakitimiza kwa uhakika maazimio yote yaliyofikiwa katika mkutano mkuu wa wanahisa wa mwaka uliopita.

 

Alisema moja ya maazimio ya mkutano huo ilikuwa ni benki kutanua wigo wake na kuwa na mawakala Dar es Salaam na mikoani huku azimio lingine likiwa ni kupunguza kiwango cha mikopo chechefu.

 

“Hayo tuliyachukua na sasa tuna mawakala nchi nzima na vituo vidogo vya kutolea huduma vitano na matawi manane huku tukifanya vizuri katika kupunguza mikopo chechefu kwa kuchukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na
kuimarisha kitengo cha ukusanyanyi madeni na kudhibiti mawakala wanaokusanya madeni na kuweka utaratibu mzuri ili mikopo inayotolewa ikidhi taratibu zilipo.

“Matokeo ya hatua hizi ni kuwa tumepunguza mikopo chechefu kwa asilimia 19 mwaka 2018 hadi asilimia 14 mwaka 2019 na pia tumepunguza uhamaji wa mikopo kutoka mikopo safi kwenda chechefu kutoka asilimia 2.6 hadi 0.3 mwaka 2019 na tunaendelea kuhakikisha kwamba mikopo inayotolewa inakuwa na
uhakika wa kurejeshwa”, aliongeza mkurugenzi huyo.

 

 

Akizungumza utendaji wa kifedha, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Fedha ya DCB, Ester Bgoya alisema moja ya sababu inayochangia benki kufanya vizuri ni kupungua kwa gharama za uendeshaji kwa mwaka jana kutoka shs bilioni 17 hadi bilioni 15.8 kunakotokana na udhibiti wa matumizi yasiyo ya lazima pamoja na kuboresha shughuli zao za uendeshaji wa biashara kwa kutumia teknolojia.

 

“Pamoja na kuwa tumekuwa na ongezeko la mikopo mwaka 2019 mapato ya riba yanaonekana kushuka kutoka shs bilioni 15.7 hadi bilioni 12.5 kulikosobabishwa na kushuka kwa riba za mikopo ikiwa ni malengo ya benki kushusha na kutoa mikopo nafuu,” alisema Bi. Ester.

 

Leave A Reply