The House of Favourite Newspapers

Wananchi 103 Mbaroni kwa Maandamano

Polisi nchini Uganda, imesema imewakamata watu 103, katika maandamano yaliozuka ya kupinga kukamatwa kwa mbunge wa upinzani Robert Kyagulanyi au Bobi Wine, pamoja na wabunge wengine kadhaa na wanaharakati nchini Uganda, huku taarifa za awali zikisema kuwa mtu mmoja ameuwa katika purukushani hiyo.

 

Vikosi vya usalama nchini Uganda, vilizima maandamano kwenye mji mkuu hapo jana Kampala, kupinga kukamatwa kwa Bobi Wine ambapo waandamanaji  wamechoma moto magurudumu ya magari, wamerusha mawe huku pia wakiweka vizuizi vya barabarani.

 

Bobi Wine, alikamatwa na kushtakiwa kwenye Mahakama ya kijeshi wiki iliyopita kufuatia madai kuwa alikuwa anamiliki silaha kinyume cha sheria ingawa wengi wanayaona mashataka hayo kama yaliyochochewa kisiasa.

 

Wanajeshi na Polisi, walionekana wakiwa juu ya magari wakipita kati kati mwa mji. Sehemu nyingine za mji wa Kampala,  maafisa wa usalama wamefyatua risasi hewani na kurusha mabomu ya machozi kutawanya waandamanaji.

 

Misukosuko inaongezeka mjini Kampala, kufuatia kukamatwa kwa mbunge Bobi Wine. Ripoti zimeibuka kuwa aliteswa akiwa mikononi mwa wanajeshi lakini Rais Yoweri Museveni,  amekana madai kuwa Bobi Wine alijeruhiwa.

 

Watu kadhaa wamekamatwa akiwemo mwandishi wa habari wa Shirika la Reuters la London, nchini Uingereza aliyekuwa akifuatilia ghasia hizo.

 

Wiki iliyopita Bobi Wine ambaye ana umri wa miaka 32, na watu wengine walishtakiwa baada ya kampeni za kuelekea uchaguzi mdogo eneo la Arua Kaskazini mwa nchi ya Uganda, na Polisi wanasema walikuwa wamewaongoza wafuasi wao kushambulia msafara wa Rais Museveni.

Comments are closed.