Wananchi Kibiti Wamshukuru Rais Samia Ujenzi Daraja la Mbuchi
WAKAZI wa Kata za Mbuchi na Mbwera Kibiti Mkoani Pwani wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa daraja la Mbuchi linalounganisha kata hizo ambalo limegharimu shilingi bilioni 7.2.
Wamezungumza hayo leo (Jumatatu, Novemba 28, 2022) wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotembelea kukagua ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa mita 61.
Wakizumgumza kwa nyakati tofauti wananchi hao wamesema kuwa ujenzi wa daraja hilo umesaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa adha ya usafiri kati ya kata hizo ambapo awali iliwalazimu kutumia mitubwi ambayo ilikuwa tishio kwa uhai wa wakazi hao hasa kipindi cha mvua kubwa mto huo ukiwa imejaa.
“Sisi kina mama tuliteseka kwa muda mrefu sana, safari za kwenda kufuata huduma za afya kwetu ilikuwa ni mtihani mkubwa, tulihofia maisha yetu, lakini kwasasa hata usiku wa manane tunavuka bila shida kufuata huduma za afya, tunamshukuru sana Rais wetu kwa kuiona changamoto yetu na kuifanyia kazi”
Akizungumza na wanamchi baada ya kukagua ujenzi wa daraja hilo, Mheshimiwa Majaliwa amewataka wakazi hao kulitumia daraja hilo kujiimarisha kiuchumi kwa kujishughulisha na kazi mbalimbali kwakuwa usafiri kwenye eneo hilo umekuwa wa uhakika kwa muda wote.
Aidha, Waziri Mkuu amewataka wakazi hao kuwa walinzi namba moja wa miundombinu kwenye daraja hilo ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kutekeleza malengo yaliyokusudiwa ya ujenzi wa daraja hilo.
Kwa upande Mwingine, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza viongozi wa mikoa kuhakikisha wanachukua hatua za kisheria mfugaji ambaye ameshindwa kufuata Sheria za nchi na kuamua kulisha mifugo kwenye mashamba ya wakulima.