The House of Favourite Newspapers

Wananchi Mkuranga Wamwangukia Magufuli Suala la Ardhi

Hassan Mohammed, mwanakijiji mwingine wa vijiji hivyo anayemlalamikia mwekezaji huyo, akiongea kwa msisitizo jambo.

BAADHI ya wananchi wa vijiji vya, Lugwadu, Magodani na Kazole, Kata ya Vikindu, Mkuranga Mkoa wa Pwani wameonyesha hisia zao kwa Rais Magufuli wakimtaka aingilie kati  mgogoro kati yao na mwekezaji waliyemtaja kwa jina la Bharmal aliyedaiwa kujimilikisha ekari 750 za ardhi.

 

 

 

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, mmoja wa wanakijiji hao ambaye yupo katika kamati ya ufuatiliaji wa migogoro hiyo, Lugano Mwamakamba,  alisema kuwa awali mwekezaji alidaiwa kumiliki ekari 1,000 kihalali lakini imepita zaidi ya miaka 20 pasipo kuziendeleza kwenye kijiji hicho cha  Kazole, ambapo alivamia ekari nyingine 750 ambazo ni mali ya wananchi.

Mwenyekiti wa kamati ya ufuatiliaji migogoro hiyo, Lugano Mwamakamba (kushoto), akizungumza na wanahabari. Pembeni yake ni baadhi ya wanavijiji hivyo.

Alifafanua kuwa katika kuvuka kijiji kimoja na kingine ni lazima upite katika shamba hilo, lakini kutokana na uvamizi huo mwekezaji huyo amekuwa hataki wananchi kupita kwenye njia ambazo zipo katika shamba hilo na walinzi wa eneo hilo wamekuwa wakiwapiga wananchi na kuwanyang’anya mali zao, jambo ambalo limewafanya leo kuzungumza na wanahabari juu ya kero hiyo ili iweze kumfikia Rais John Magufuli.

Alisema kuwa juhudi za kumtafuta Waziri wa Ardhi Nyumba na Makazi,   Wiliam Lukuvi,  zilishafanyika lakini cha kushangaza hawajapata msaada wowote, na si tu kwa waziri huyo bali hata katika viongozi wa serikali wa wilaya hiyo ambao waliwafikishia kero hizo  na kuambiwa kuwa mwekezaji huyo anamiliki kihalali eneo hilo la ekari 1,750.

Mtandao huu umefanya juhudi za kumtafuta Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo,  ili kuzungumzia suala hilo lakini simu yake ya mkononi iliita bila kupokelewa na alipotumiwa ujumbe wa maneno haukujibiwa.

Mkutano na wanahabari ukiendelea.

Na Denis Mtima/GPL

Comments are closed.