The House of Favourite Newspapers

Wananchi……. The Return of Champions

0

KABLA ya kuanza kwa mchezo wa juzi Jumamosi kati ya Simba na Yanga, mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele, alisema: “Natamani kuifunga Simba.”

 

Matamanio ya mshambuliaji huyo mpya wa Yanga raia wa DR Congo, yalitimia dakika ya 12 ya mchezo huo wa Ngao ya Jamii uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar, baada ya kufunga bao pekee lililoipa ushindi timu yake wa 1-0.

 

Mayele alifunga bao hilo akimalizia pasi nzuri ya winga, Farid Mussa aliyepata pasi ndefu akiwa pembeni kutoka kwa kipa wake, Djigui Diara kabla ya kuingia ndani na kumpatia mfungaji aliyewainua vitini mashabiki wa Yanga.

 

Kuingia kwa bao hilo, kuliwachanganya Simba ambapo akili mwao ikaja taswira ya Julai 3, mwaka huu pale Zawad Mauya alipofunga bao dakika ya 12 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara zilipokutana timu hizo na mchezo kumalizika kwa Yanga kushinda 1-0 kama ilivyokuwa juzi.

 

Katika mchezo huo wa juzi, Yanga iliuanza kwa kasi sana ambapo mashambulizi yao ya mara kwa mara, yaliwapa faida ya bao hilo la mapema na kuwavuruga Simba.

 

Simba ilishuhudiwa mapema dakika ya 26, ikimpoteza beki wake mahiri, Joash Onyango aliyetolewa uwanjani na kuingia Kennedy Juma baada ya kuumia.

 

Wakati mapema tu Onyango akitoka kwa kuumia, dakika chache kabla ya kumalizika kwa mchezo huo, kiungo wa Simba, Taddeo Lwanga, alitolewa uwanjani baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano iliyoambana na nyekundu kutokana na kufanya faulo.

 

Mchezo huo ulikuwa ni wa ufunguzi wa msimu wa soka 2021/22 Tanzania ambapo Septemba 27, mwaka huu, Ligi Kuu Tanzania Bara inatarajiwa kuanza kwa kuzishirikisha timu 16.

 

Kabla ya mchezo wa juzi, timu hizo zilikutana mara ya mwisho mwaka 2017 katika Ngao ya Jamii na Simba ikaibuka na ushindi wa penalti 5-4 baada ya muda wa kawaida kushindwa kufungana.

 

Taji walilolipata Yanga juzi, limefungua njia ya kubeba mengine msimu huu wa 2021/22 ambapo mwanzoni waliingia na kauli mbiu ya The Return of Champions wakimaanisha kurejea kwa mabingwa.

 

SIMBA WALIKOSEA HAPA

Kipindi cha kwanza, Simba walikosa utulivu baada ya Onyango kutoka hali iliyowafanya kushindwa kuanzisha mashambulizi yaliyowapa shida Yanga.

 

Mbali na hivyo, kipindi cha pili, safu yao ya ushambuliaji ilipaniki, huku ikiwa butu ikiambulia shuti moja pekee lililolenga lango lililopigwa na John Bocco. Kulingana na mchezo jinsi ulivyo, Simba kufanya makosa hayo ndiyo chanzo kikubwa cha kupoteza mbele ya Yanga.

 

VITA YA WACHEZAJI

Mchezo huo ulikuwa na vita kubwa ya wachezaji wa pande zote mbili hasa wale wapya ambapo hadi unamalizika, ilionekana wale wa Yanga kufanya vizuri zaidi.

 

Kwa upande wa wachezaji wa Simba, kipa Aishi Manula, alifanya sevu nane, lakini alishindwa kuzia shuti la Mayele na kuruhusu bao.

 

Kiungo mpya Pape Ousmane Sakho, alifanya dribo 17, huku akipiga pasi 20, akajikuta akichezewa faulo tatu na kupiga shuti moja lililolenga lango. Kwa upande wa kiungo Sadio Kanoute, alifanya dribo 20, alipiga pasi 35, alichezewa faulo 4.

 

Rally Bwalya, alipiga pasi 34, huku akidribo mara sita na kupiga mashuti manne yasiyolenga lango. Ukija kwa Yanga, kiungo Khalid Aucho, alimaliza mchezo kwa kupiga jumla ya pasi 46, ambapo 38 zilifika kwa usahihi na nane hazikufika kwa walengwa. Yeye ndiye alionekana kuwa hatari zaidi kushinda wote akifanya balaa zito.

 

Ukiachana na yeye, Yannick Bangala Litombo, aliwafunika vilivyo Kanoute na Sakho baada ya kupiga jumla ya pasi 38. Diara alilinda lango lake vizuri akifanya sevu tisa. Mfungaji wa bao pekee, Mayele, alipiga mashuti mawili, moja lililenga lango na kuwa bao, huku lingine likitoka nje.

 

MANARA APAGAWA, AVUA SHATI

Msemaji wa Yanga, Haji Manara, ushindi wa juzi ulimpagawisha vilivyo kwani baada ya filimbi ya mwisho kupulizwa, aliingia uwanjani kushangilia na wachezaji huku akiwasalimia mashabiki wa timu hiyo.

Wakati akiendelea kufanya hivyo akiwa na walinzi wake, alivua nguo yake ya juu aliyovaa bila ya kujali chochote.

 

NABI ANACHEKA TU

Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi, alionekana kucheka muda wote baada ya mchezo kumalizika kutokana na kuwapa furaha Wanayanga.

Hii inakuwa ni mara ya pili kwa Nabi kuifunga Simba tangu akabidhiwe kikosi hicho ambapo amepambana nayo mara tatu, akipoteza moja faina ya Kombe la Shirikisho la Azam.

 

REKODI ZAO NGAO YA JAMII

Kuanzia 2001, Simba na Yanga zimekutana mara tano kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii, Yanga imeshinda tatu na Simba mbili, huku timu zote zikibeba taji hilo sawa, kila moja mara sita kuanzia 2001 hadi 2021.

 

KIKOSI CHA SIMBA KILICHOANZA

Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohamed Husein, Joash Onyango, Pascal Wawa, Taddeo LWanga, Pape Sakho, Sadio Kanoute, Chriss Mugalu, Rally Bwalya na Hassan Dilunga.

 

KIKOSI CHA YANGA KILICHOANZA

Djigui Diarra, Djuma Shaban, Kibwana Shomari, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Khalid Aucho, Moloko Jesus, Yannick Bangala, Fiston Mayele, Feisal Salum na Farid Mussa.

 

Kwa mwaka 2021 pekee, Yanga na Simba zimekutana mara nne kwenye michuano tofauti. Yanga imeshinda tatu, Simba moja.

PICHA: MUSA MATEJA NA IBRAHIM MUSSA, Dar es Salaam

 

Leave A Reply