Wananchi wa Igalula Sengerema waanza kulipwa fidia kupisha shughuli za Mgodi
Zaidi ya Shilingi Bilioni 60 zinatarajiwa kulipwa kwa wanufaika 853 kwenye Vijiji vya Sotta na Nyabila kata ya Igalula- Sengerema ili kupisha shughuli za uchimbaji Madini kwenye Mgodi wa Nyanzaga unaomilikiwa kwa Ubia Kati ya Kampuni ya Ore Corp Limited (84%) na Serikali ya Tanzania (16%).
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi akiwa kwenye hafla ya kukabidhi mfano wa Hundi yenye thamani ya zaidi ya Bilioni 3.7 ambazo zimeshalipwa kwa wanufaika ikiwa ni ishara ya kuendelea kwa zoezi la ulipaji fidia kwa wanaopisha shughuli za uchimbaji madini.
Amesema, wanufaika 152 sawa na asilimia 17.8 ya ambao hawajasaini mikataba ya fidia wanapaswa kufanya hivyo na kujiandaa kupisha kwenye maeneo na hata wanaojengewa nyumba kufanya hivyo mara tu watakapopata nyumba zao na kwamba serikali ipo bega kwa bega kusimamia haki za wananchi na mwekezaji kwa manufaa ya Taifa.
Makilagi amesema hatua iliyofikiwa na ulipaji wa Fidia kwa wananchi ni ishara njema ya kuanza rasmi kwa shughuli za uchimbaji kwenye eneo hilo hivyo ni wajibu wa wanufaika walichangamkie fursa hiyo na akatoa wito kwa wananchi wa Sengerema kujiandaa na fursa za kiuchumi kama ajira na kufanya biashara kutokana na uwepo wa Mgodi huo uliowekeza zaidi ya Trilioni 1.
Hata hivyo, ametoa wito kwa kampuni hiyo na makampuni mengine Madogo yaliyoingia mkataba na kampuni mama kuhakikisha wanatekeleza vema sheria ya kurejesha faida kwa jamii inayowazunguka na ushuru wa huduma kwa kulipa kodi zote stahiki kwa serikali kuu kupitia Mamlaka ya mapato nchini (TRA) na ile ya halmashauri.
“Kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu kumekua na mabadiliko ya Tabia nchi hivyo natoa wito kutochafua vyanzo vya maji na kuhakikisha mnatunza mazingira na mnalilinda ziwa letu na mjiepushe na ukataji wa miti ili kuepusha athari za kimazingira na wananchi naomba tujenge tabia ya kupanda miti”alisema Makilagi.
Akizungumzia utekeleaji wa mpango wa uhamishaji watu na makazi, msimamizi wa miradi ya kampuni hiyo nchini Isaac Lupokela amesema hadi Septemba 02, 2023 waguswa 701 wameshapata ufafanuzi wa stahiki zao na wamekwisha saini mikataba na kwamba mikataba 190 imekamilika na kuchukuliwa na waguswa na uelimishaji unaendelea.
“Tunaendelea na kazi ya Ujenzi na utaajiri maelfu ya watanzania wa maeneo ya jirani ambapo tunatarajia kuwaajiri zaidi ya watu elfu moja na zitakuwepo pia ajira za muda, zoezi la uchimbaji dhahabu litakua na manufaa kwa Sengerema na Taifa kwa ujumla, na fedha za ulipaji fidia tayari zipo kwenye akaunti.” Amefafanua bwana Lupokela.
Amefafanua kuwa leseni namba 653 ya mwaka 2021 iliwapa kampuni hiyo eneo lenye ukubwa wa Hekta za Mraba 23. 4 na kwamba kwakua kulikua na Kaya zinazoishi ndani ya eneo hilo walipashwa kufanya uthaminishaji ili kulipa fidia stahiki kabla ya kutwaa ardhi hiyo kwa mujibu wa sheria jambo ambalo linafika mwisho siku za usoni.