The House of Favourite Newspapers

Wananchi Wakusanyika Airport Mtwara, Kimbunga Chatua Comoro – Video

 

MVUA za wastani zisizokuwa na upepo zimeendelea kunyesha katika maneo mbalimbali mkoani Mtwara huku  wananchi wakiwa wamajikusanya katika maeneo maalum yaliyotengwa katika tahadhari dhidi ya kimbunga kiitwacho Kenneth kinachotegemewa kutokea Msumbiji.

 

Maeneo hayo ni Uwanja wa Ndege wa Mtwara, eneo la Jeshi la Wananchi nchini (JWTZ) Kikosi cha Naliendelee, Shule za Majengo, Tandika, Mitengo, Sabodo na Sabasaba.

Mjini Lindi, asubuhi leo palinyesha mvua ndogo na wananchi wameendelea na shughuli zao kama kawaida. Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godffrey Zambi aliamuru kusitishwa kwa shughuli zote za Serikali, wafanyakazi wote wa serikali na mashirika ya umma kutokwenda kazini leo kufuatia tahadhari ya Kimbunga hicho huku akitangaza pia kusitisha maadhimisho ya Siku ya Malaria Duniani ambayo Kitaifa ilipangwa kufanyika leo mkoani Lindi.

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), Dkt Agnes Kijazi,  ametaja athari zinazoweza kutokea kutokana na kimbunga  hicho.

“Kwa wakazi wa Mtwara kuna mvua zinaendelea kunyesha na hizo mvua kwao wataona ni za kawaida lakini sio za kawaida, kesho kimbunga kitatua Msumbiji, lakini baada ya hapo kitaondoka na baadaye kitarudi tena baharini.

“Leo asubuhi Kimbunga Kenneth kilikuwa kimefika karibu kabisa na pwani ya nchi yetu na pwani ya Msumbiji, kimeshakuwa kimbunga chenye nguvu kubwa zaidi, na kinavyosogea maeneo ya pwani kinaongezeka nguvu, sasa hivi kipo visiwa vya Comoro.

“Kesho tarehe 26 Aprili, alfajiri, kimbunga hiki kitatua nchi kavu na katika ardhi ya Msumbiji, kitakuwa umbali wa kilomita 237 kutoka eneo la pwani ya Mtwara,” alisema.

Aidha, wavuvi mkoani Mtwara wameitikia wito wa serikali wa kutojihusisha na shughuli za uvuvi leo kufuatia tahadhari ya kuwepo kwa kimbunga cha Kenneth iliyotolewa na TMA na kusisitizwa na mkuu wa mkoa huo.

Comments are closed.