The House of Favourite Newspapers

Wananchi Wasilishwe Vibudu; Serikali Isimamie Hilo

KITOWEO kinatumika na watu wengi mijini na vijijini, ni bidhaa inayohitaji kuwa safi na salama wakati wa utayarishaji wake kuanzia wakati wa kuchinja hadi inapouziwa.

 

Kutokana na hilo ni wazi kwamba inapochinjwa ni lazima mamlaka husika zifuatilie na kujiridhisha kuwa nyama hiyo inafaa kuliwa na haiwezi kuleta madhara ya kiafya kwa walaji. Ndio maana wauzaji wakawekewa utaratibu wa kuisafirisha nyama kwa kutumia magari maalumu na siyo ilimradi usafiri.

 

Kutokana na ukweli kwamba biashara ya nyama kuhitaji umakini wa hali ya juu, wataalamu wa mifugo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na maofisa wa afya wa halmshauri za wilaya na manispaa wanakuwa na jukumu la kufuatilia kwa karibu biashara hiyo.

 

Tukio la kukamatwa kwa nyama ya ng’ombe waliokufa iliyokuwa kwenye mpango wa kuingizwa sokoni jijini Dar es Salaam, linaashiria kuwa nyama inayouzwa katika baadhi ya sehemu nchini ni ya vibudu na siyo salama kwa afya za binadamu kwa sababu hazijapimwa.

 

Kutokana na tukio hilo Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya Waziri Luaga Mpina ilitangaza kuyafunga baadhi ya machinjio kama vile ya Tegeta, Dar na kuagiza mmiliki wake kukamatwa kwa kile kilichoelezwa ni kuwapo kwa nyama za ng’ombe waliokufa iliyokuwa inaingizwa sokoni.

 

Waziri Mpina alisema wiki iliyopita kuwa uamuzi huo ulifikiwa baada ya timu ya wizara kufanya uchunguzi na kubaini ujanja wa kuuza nyama ya ng’ombe waliokufa ambao walikutwa wameshachinjwa na kutaka kuchanganywa na waliokufa kwa kuchinjwa. Kwa mujibu wa Mpina, mfanyabiashara mmoja alipeleka ng’ombe kwa ajili ya kuchinjwa, baadhi wakiwa hai na wengine wamekufa kiasi cha kuharibika kabisa na kutoa harufu.

 

Akasema ng’ombe hao waliokufa walishushwa kwenye lori na kuwachinja na wakataka kuwachanganya na nyama za kawaida, akasmakabla ya kufanya hivyi, wizara ilipata taarifa na kuwahi wasichanganywe na timu ya operesheni iliyopo Dar ilipata taarifa na kukamata lori na mizoga ya ng’ombe ambayo baadaye ilipelekwa kuteketezwa.

 

Lakini isiishie hapo ni lazima gari na dereva aliyeruhusu uchafu huo wasaidie vyombo vya dola kueleza njama hizo zimefanywa kwa siku ngapi na je ni Dar tu ambako wanalishwa watu vibudu? Mimi naamini wote waliohusika na uchafu huo wakihojiwa watasaidia kutoa taarifa zaidi zitakazosaidia mamlaka husika kujipanga katika kudhibiti na kusimamia biashara ya nyama.

 

Kifupi tukio hili ni somo kubwa na kinaonesha kuna mianya mingi inayotumiwa na wafanyabiashara kuwauzia wananchi nyama isiyofaa kwa matumizi yao. Naamini kutokana na tatizo hili, Waziri Mpina atakaa na watendaji wake ili kudhibiti uingizwaji wa nyama isiyofaa kuliwa sokoni.

 

Njia sahihi ni kufanya ukaguzi wa kila siku wa nyama ambazo wanauziwa wananchi kwenye maduka ya nyama na kama kuna watu watakaofanya ufisadi wa kuwauzia wananchi nyamba mbaya basi sheria ichukue mkondo wake.

STORI: ELVAN STAMBULI.

Comments are closed.