Wananchi Watakiwa Kuwa Mabalozi Kwenye Mapambano Dhidi Ya Ajali Za Barabarani
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Daniel Sillo amewataka wananchi wote bila kujali jinsia kujitolea kwa kuwa mabalozi katika kuzuia ajali za barabarani zinazosababisha vifo, majeruhi na wakati mwingine ulemavu wa kudumu.
Sillo ameyasema hayo Septemba 28, 2024 mkoani Iringa kwenye Maadhimisho ya miaka kumi ya Shirika la Mabalozi wa Usalama barabarani Tanzania toka kuanzishwa kwake ambapo wadau mbalimbali wa usafirishaji na wananchi wamehudhuria.
Aidha, akizungumza kwenye hafla hiyo ambayo imehudhuliwa pia na askari kutoka Jeshi la polisi, Zimamoto na uhamiaji, Sillo amesema kuwa, jamii inapaswa kutambua mapambano dhidi ya ajali za barabarani ni jukumu letu sote hivyo tunapaswa kukumbushana, kutoa elimu lakini pia kukemea vitendo vya uvunjaji wa Sheria za usalama barabarani.
Ameongeza kuwa, madhara makubwa ya ajali za barabarani huwakumba wanawake na watoto kwani takwimu zinaonyesha kwamba mara nyingi vifo vingi huwakumba wanaume, baba anapofariki watoto wanabaki yatima mke anabaki kuwa mjane na pia anachukua majukumu ya kuendesha familia kitendo kinachopelekea kuwepo kwa watoto wa mtaani.
“Nitoe rai kuanzia kwa Mkuu wa Kikosi cha usalama barabarani nchini, wakuu wa usalama barabarani wa mikoa na askari wote kuwaunga mkono mabalozi wa usalama barabarani katika shughuli zote za usalama barababarani” – Naibu Waziri Sillo.
Naye kwa upande wake Kamishna wa polisi (CP) Shabani Hiki ambaye amemuwakilisha Mkuu wa Jeshi la polisi nchini (IJP) Camillus Wambura amesema kuwa, Mabalozi wa usalama barabarani wana mchango mkubwa kwenye jamii hasa kwa Jeshi la Polisi kwani wamekuwa wakijitoa kufanya kazi za usalama barabarani bila malipo yoyote, amewataka kuendelea kutoa elimu ili kuzidi kuelimisha jamii kuhusu sheria za usalama barabarani kwani jukumu letu sote.
Ifahamike kwamba, Shirika hilo la Mabalozi wa usalama barabarani (Road Safety Ambassadors) tangu kuanzishwa kwake limekuwa likijishughulisha na utoaji wa elimu kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu Usalama barabarani na kupewa ushirikiano mkubwa kutoka Jeshi la polisi Kikosi cha usalama barabarani Tanzania.