WANANDOA BONGO WALIONASWA KWA MADAWA YA KULEVYA…MAPYA YAANIKWA!

NYUMA ya matukio ya wanandoa kunaswa kwa tuhuma za biashara ya madawa ya kulevya, kuna mambo mapya yameanikwa, Uwazi limedokezwa. 

 

Tukio bichi ni la kukamatwa kwa wanandoa, mfanyabisahara maarufu jijini Dar es Salaam, Abdul Nsembo almaarufu Abdukandida (45) na mkewe Shamim Mwasha waliokamatwa Mei Mosi, mwaka huu wakidaiwa kukutwa na dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa zaidi ya gramu 400.

 

Nsembo na Mwasha ambaye ni mwanahabari na mmiliki wa maduka na Blogu ya 8020fashion walitiwa nguvuni nyumbani kwao, Mbezi-Beach jijini Dar es Salaam na maofisa wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) iliyo chini ya Kamishna Mkuu, Rogers Siyanga.

 

Hadi sasa, kwa mujibu wa Kamishna wa Operesheni wa DCEA, Luteni Kanali Frederick Milanzi, wanandoa hao wanashikiliwa na Jeshi la Polisi nchini hadi upelelezi utakapokamilika ndipo wafikishwe mahakamani.

 

WANANDOA WENGINE

Ukimwacha Nsembo na Mwasha, Januari 19, 2018, wanandoa wengine kutoka Tanzania, Baraka Malali na mkewe Ashura Musa nao walikamatwa kwa tuhuma za dawa za kulevya kwenye Uwanja wa Ndege wa Baiyun, Guangzhou nchini China. Wawili hao walikamatwa na pipi 129 za dawa hizo za kulevya aina ya heroin ambapo hadi leo kesi yao inaendelea nchini humo.

MAPYA YAANIKWA

Kufuatia kesi nyingi kuhusisha mume na mke, kumeibuka swali la kwa nini huwa wanakamatwa wote na kuacha watoto wakiteseka?

 

UWAZI NA MAMLAKA

Juu ya suala hilo, Gazeti la Uwazi lilizungumza na mamlaka hiyo ya kuzuia na kupambana nadawa za kulevya na kufunguka usiyoyajua.

 

Kwa mujibu wa ofisa mmoja wa mamlaka hiyo aliyeomba jina lake lisiandikwe gazetini, kunapokuwa na tuhuma za kujihusisha na biashara hiyo haramu, wote huwa wanakamatwa kwa sababu wanaishi na wanalala wote chumba kimoja, yaani wapo pamoja hivyo lazima waambizane siri zao. “Ukweli ni kwamba msiri wa mume ni mke, kwa sababu huwa ni mwili mmoja,” alisema sosi huyo.

 

KOSA LA MKE

“Wakati mwingine utakuta mke hausiki, lakini kosa lake linakuwa hakutoa taarifa kwenye vyombo vya dola, sasa kiushahidi, lazima akamatwe, akaeleze anachokijua. “Wakati mwingine inawezekana kukawa na upelelezi wa awali unaokuwa umefanyika na kugundua jambo, ndiyo maana akikamatwa mume, basi na mke wake, anakamatwa.

 

“Wakati mwingine mtuhumiwa anaweza akawa ni mume, lakini kutokana na mazingira na namna mke anavyotoa ushirikiano, ama kwa kumficha, lazima akamatwe, aeleze anachokijua au kwa nini alikuwa anamficha au kuficha siri zake,” alisema ofisa huyo.

 

MKE AKIWA HAJUI

Gazeti la Uwazi lilipotaka kujua endapo wanandoa hao wameoana muda mfupi halafu mke akawa hajui kama mumewe anajihusisha na biashara hiyo haramu inakuwaje? Ofisa huyo akajibu: “Anakamatwa kwa lengo la kusaidia Polisi katika upelelezi.”

ANAYEHUSIKA ANAJULIKANA

“Kwenye tuhuma hizi ndiyo maana kunakuwa na wapelelezi halafu kuna mahakama kwa ajili ya kutoa haki. Halafu maelezo ya anayejua na asiyejua yanaonekana tu katika kuhojiwa wakati wa uchunguzi. Mara nyingi wasiohusika huwa wanaachiwa na mhusika anabeba msalaba wake.

 

“Wakati mwingine mmoja wa wanandoa hukaa mahabusu kwa ajili ya usalama wake tu, lakini pia kama alikuwa anajua madhabi hayo huwa tunajiuliza kwa nini alikuwa hadai talaka, akakaa mbali na uhalifu huo?” alihoji ‘sosi’ huyo.

 

Juzi Jumapili, Uwazi lilimtafuta Msemaji wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kelevya, Florence Bahati ili kupata kwa kina ‘ishu’ ya wanandoa kujihusisha na biashara hiyo haramu lakini alisema kuwa jambo hilo angelizungumzia kamishna wa mamlaka hiyo jana, Jumatatu.

 

Awali Kamishna wa Operesheni wa DCEA, Luteni Milanzi aliiambia Uwazi kuwa Abdukandia na mkewe Shamim walikamatwa baada ya polisi kupewa taarifa zao na raia wema. “Shamim alipofungua geti aliwaambia maafisa wa DCEA kuwa mumewe amesafiri siku tatu zilizopita lakini alipopekuliwa nyumbani humo alikutwa juu kwenye dari akiwa amejificha,” alisema kamishna huyo.

 

Milanzi alidai mtuhumiwa huyo ana mtandao mkubwa wa kimataifa na wana majina ya watu wanaoshirikiana nao kutoka nchi za Brazil,Ulaya, Asia na Afrika. Alisema watuhumiwa hao wanashikiliwa kwa ajili ya upelelezi na ukikamilika watafikishwa mahakamani.

 

Licha ya kukamatwa kwa wanandoa hao, kuanzia Februari hadi Aprili mwaka huu, watu saba wamekamatwa mkoani Tanga wakidaiwa kuwa na dawa za kulevya aina ya heroine zenye uzito wa kilo sita na tayari wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.


Loading...

Toa comment