WANAODAIWA KUMUUA TAJIRI, KAMANDA AFICHUA MIKATE ILIVYOWAPONZA

Watuhumiwa wakiwa chini ya ulizni.

 

MBEYA: kufuatia kuuawa kwa kupigwa risasi kichwani hivi karibuni kwa mfanyabiashara maarufu wa madini wa Kitongoji cha Kasanga Kanyika, Kijiji cha Lupa, wilayani Chunya mkoani Mbeya, Mwile Sinjale (40), Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, DCP Mohammed Mpinga (pichani) amefichua siri ya mikate ilivyowaponza wanaodaiwa kuua.

 

Akizungumza na mwandishi wetu kufuatia tukio hilo lililofanya wananchi wengi kutaka kujua kilichoendelea baada ya mauaji hayo yaliyotokea mchana kweupe saa tisa alasiri, Kamanda Mpinga alisema polisi walikuwa katika upelelezi mkali na uchunguzi wao umebaini kwamba majambazi hao walitumia bunduki aina ya Shotgun.

Alisema mfanyabiashara huyo alikuwa akitokea Chunya mjini kwa kutumia usafiri wa pikipiki yake akiwa amepakiwa na mfanyakazi wake na alikuwa amebeba mikate mikubwa miwili kwenye mkoba mgongoni, hivyo watuhumiwa hao walidhani amebeba pesa.

 

Aliongeza kuwa watuhumiwa hao wa ujambazi baada ya kuona mfuko umetuma, walimvamia na kumpiga risasi kichwani na kumuua kisha kutokomea na mfuko huo uliokuwa na mikate.

Kamanda Mpinga alisema katika upelelezi wao walibaini kuwa tukio hilo lilifanywa na watu wanne wanaume ambao walikuwa na bunduki hiyo na mapanga matatu huku nyuso zao zikiwa zimefunikwa kwa kitambaa cha kuziba uso (maski).

 

Vifaa walivyopkamatwa navyo.

 

 

“Baada ya tukio hilo, watu hao walifanikiwa kutokomea porini na jeshi la polisi likaingia kazini kuwatafuta na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wa ujambazi wawili kati ya wanne ambao wanadaiwa kuhusika katika tukio hilo lililotokea Januari 31 mwaka huu,” alisema.

Akifafanua zaidi Kamanda Mpinga alisema baada ya mahojiano, watuhumiwa hao, Fitina Ruben (30) na Sumbuko Sanga (32), wote wakazi wa chunya wamekiri kuhusika na mauaji ya mfanyabiashara huyo wa madini.

Akaongeza kuwa baada ya kukamatwa na kufanyiwa upekuzi, watuhumiwa hao walikutwa na silaha na vitu mbalimbali ambavyo huvitumia katika uhalifu.

 

Alizitaja silaha na vitu walivyokutwa navyo kuwa ni bunduki moja aina ya shotgun iliyotengenezwa kienyeji, risasi moja inayotumiwa na silaha aina ya shotgun, manati moja, mask tatu, rungu moja na panga moja.

Vingine ni nondo moja, koti moja la kijeshi, gloves moja, mzula mmoja na simu moja aina ya tecno ambayo mmiliki wake bado hajafahamika.

 

Kamanda Mpinga ametoa onyo kali kwa yeyote atakayejihusisha na uhalifu akisema kuwa Jeshi la Polisi halitakuwa na huruma katika kuwashughulikia kwa kuchukua hatua za kisheria.

Pia ametoa rai kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuzuia uhalifu ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za mtu/watu au kikundi cha watu wanachokitilia shaka ili upelelezi ufanyike dhidi yao.

STORI: MWANDISHI WETU, MBEYA

Loading...

Stori zinazo husiana na ulizosoma

Toa comment