The House of Favourite Newspapers

Wanaotumia Bima za NHIF za Ndugu Zao Waonywa

0

MENEJA wa Mfuko wa Taifa wa Mima ya Afya (NHIF) Jijini Mwanza, Jarlath Mushashu, amewaonya wananchi mkoani hapa ambao wana tabia ya kutumia kadi ya bima ya afya ambazo si za kwao waache mara moja kwani ni kosa kisheria na wanahujumu uchumi wa Serikali.

 

 

Mushashu amesema hayo wakati wa mkutano na wanahabari na kuongeza kuwa wananchi wajiwekee utaratibu wa kukata bima za afya na waachane na kutumia bima za watu wengine ili kujiepusha na matatizo ambayo yanaweza kuwakumba ikiwemo kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

 

 

Amewasihi wananchi kufuata taratibu za matibabu ya afya, ili kuepukana na changamoto ya kupata magonjwa kwa kutumia dawa kiholela bila maelekezo ya wataalamu wa afya kwani kuna madhara makubwa kiafya ambayo yanaweza kusababisha gharama kubwa katika matibabu na hata kupoteza uhai.

 

“Baadhi ya wananchi wamekuwa wakijitibu kwa mazoea, wanakwenda kwenye maduka ya dawa na kununua dawa ambazo haziendi kutibu ugonjwa walionao, badala yake zinasababisha maradhi mengine yanayoweza kupelekea kuugua na kupoteza nguvu kazi katika jamii,” amesema.

 

 

Aidha, ameongeza kuwa NHIF inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuendelea kujiunga na mfuko huo, ambapo mpaka sasa wameshatembelea wanachama wa vyama vya ushirika AMCOS wapatao 1200 na waliojiunga ni 812 kutoka wilaya za Magu na Sengerema ili kujihakikishia matibabu wanapougua hata kama hawana pesa mfukoni.

 

 

“Kwa mujibu wa kalenda yetu kwa mwaka jana pekee tufanikiwa kutoa kadi za bima za afya zaidi ya 36,00 ambapo wanaume ni 18,261 elfu na wanawake 18,207,” ameongeza.

Na Leah Marco, Mwanza

Leave A Reply