The House of Favourite Newspapers

Wanaswa kwa kulima bangi, watiwa mbaroni

0

Stori: Stephano Mango, Songea
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma linawashikilia wakazi wawili wa Vijiji vya Mseto na Liparamba wilayani Nyasa kwa tuhuma za kukutwa wakiwa wamelima mashamba mawili ya bangi yenye ukubwa wa heka tano ambayo inadaiwa yamekuwa yakitegemewa na watu wanaojihusisha na biashara haramu ya kuuza bangi wilayani humo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Zuberi Mwombeji akizungumza na gazeti hili ofisini kwake amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Thadei Ngonyani (26) mkazi wa Kijiji cha Mseto na Philimoni Kumburu (58) mkazi wa Kijiji cha Liparamba.
Alifafanua zaidi kuwa Jeshi la Polisi mkoani humo limefanya msako katika maeneo mbalimbali dhidi ya watu wanaojihusisha na kilimo cha bangi na msako ulianza katika Wilaya ya Nyasa.

Kamanda Mwombeji alieleza kuwa katika tukio la kwanza katika Kijiji cha Mseto kilichopo Kata ya Liparamba Tarafa ya Mpepo, askari polisi wakiwa kwenye msako mkali walifanikiwa kumkamata Ngonyani akiwa amelima zao hilo la bangi lenye ukubwa wa heka tatu.

Alieleza zaidi kuwa katika shamba hilo, Ngonyani alikuwa amechanganya na mazao mengine pembeni kwa lengo la kuficha bangi ambayo ilikuwa katikati ya shamba.

Katika tukio la pili inadaiwa kuwa Kumburu alidakwa na askari polisi baada ya kubainika ana shamba la bangi lenye ukubwa wa heka mbili ambalo ndani ya shamba hilo aliotesha miche mingi ya bangi na pembeni alipanda mahindi kwa lengo la kulificha zao hilo haramu la bangi lisionekane kwa urahisi.

Alisema kuwa mara tu baada ya kuwakamata watuhumiwa hao taratibu za kuharibu bangi hiyo zilifuata sambamba na kuichoma moto chini ya ulinzi mkali wa polisi na watuhumiwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani mara tu upelelezi utakapokamilika.

Leave A Reply