WANATEMBELEA NYOTA ZA KAKA ZAO?

MUZIKI wa Bongo Fleva kila siku unazidi kuongeza sura mpya, kila anayekuja kwenye gemu huwa anakuwa na njia zake.

Wapo ambao wanasaidiwa na wadhamini mbalimbali, wapo pia wanaosaidiwa na maprodyuza na wapo pia ambao wanabebwa na kaka au ndugu zao waliotangulia kwenye ‘game’.

 

Full Shangwe leo linakumegea orodha ya wasanii ambao wanatajwa kuwa wanatembelea nyota za kaka au dada zao, wapo ambao wamefanikiwa sana lakini wengine licha ya kubebwa, wameshindwa kutoboa kimuziki:

 

ABDU KIBA

Amekuwa akijitahidi kufanya muziki wake huku mara kadhaa akimshirikisha kaka yake, AliKiba lakini jina lake limekuwa si kubwa kivile kwenye gemu la Bongo Fleva.

Amejitahidi kufanya ngoma kama Kizunguzungu lakini haukufanya vizuri sana. Alipofanya na kaka yake ngoma kama Kidela na Single, zimempa mafanikio ya kusikika lakini baada ya muda, kimyaa!

 

QUEEN DARLEEN

Huyu ni dada yake na Diamond. Licha ya kuwa ametangulia kuliona jua na kuanza muziki lakini bado Diamond alikuja kumvuka na kufanya vizuri.

Mara baada ya kutoboa, Diamond amekuwa akijaribu kumbeba dada yake huyo lakini matokeo yamekuwa ya kawaida. Yupo kwenye gemu lakini si kwenye levo za juu sana.

Queen amejitahidi kufanya ngoma kama Touch, Kijuso na Ntakufilisi lakini zote hizo hazikuweza kumuweka kwenye levo za juu sana kimuziki.

NIKI WA PILI

Huyu ni mdogo wake na mwamba wa Hip Hop kutoka Arusha, Joh Makini. Kwa upande wake anaonekana kufanikiwa. Jina alilonalo kaka yake mara kadhaa ameonekana kulikaribia kutokana na utunzi wake wa nyimbo kama Good Boy na Quality Time.

 

MAUNDA

Ni mdogo wake na Banana Zorro. Familia yao ni ya muziki kuanzia baba yake Zahir Zorro. Licha ya kufanya nyimbo zake peke yake lakini bado ilionekana Banana ndio anayempa kampani kubwa. Hata hivyo kwa muda mrefu sasa hasikiki.

Maunda amewahi kusumbua na ngoma kama Mapenzi ni ya Wawili na Nafurahi ambazo zilifanya vizuri sana lakini hata hivyo, jina lake kwa sasa limerudi chini.

TOTOO KALALA

Huyu ni mdogo wake na Kalala Junior, licha ya kuwa kwenye familia ya muziki lakini alionekana kupewa sapoti na Kalala na bahati nzuri yeye alionekana kutusua katika Bendi ya FM Academia.

MIMI MARS

Amechipukia hivi karibuni, anaonekana kuutendea haki mwanya wa kutanguliwa na dada yake, Vanessa Mdee. Mimi anasumbua na Nadata, Shuga na wimbo mpya wa Sitamani, pia ni mtangazaji wa televisheni.

Kama ataendelea na kasi aliyonayo, kuna uwezekano mkubwa akawa ameitumia nafasi vizuri na kuweza kufika kwenye levo za juu za wasanii wanaofanya vizuri Bongo Flevani.

BLACK RYNO

Ni mdogo wake na legendari wa Bongo Fleva, Profesa Jay. Licha ya juhudi zake za kuibuka kileleni mara kadhaa na ngoma kama Usipime na Black Chatta lakini ameshindwa ‘ku-maintain’ kubaki kileleni. Kaka yake ameendelea kusikika hadi leo licha ya sasa kujikita kwenye masuala ya kisiasa lakini jina lake bado lipo kwenye ramani ya Bongo Fleva wakati mdogo wake, chaliii!

MAKALA: ERICK EVARIST

Loading...

Stori zinazo husiana na ulizosoma

Toa comment