The House of Favourite Newspapers

Wanaume wazima mnaotembea na mabinti, mnaibiwa!

0

Asalam alaikum wapenzi wasomaji wangu, bila shaka mnaendelea vema na ujenzi wa taifa letu, kwa upande wangu nina amani na afya tele namshukuru Mwenyezi Mungu.

Leo nimeamua kuwaamsha wanaume watu wazima wanaotembea na mabinti ambao ni tofauti na umri wao kwa upande mwingine, nawaonea huruma kwani wanaibiwa bila kujua na pengine wanajua lakini wanashindwa kufuatilia kwa sababu wameingia kwenye penzi lisilo rasmi.

Kabla sijaandika mada hii moja kwa moja niwaulize swali, hivi mnajisikiaje mnapotembea na watoto mnaoweza kuwazaa na wakati mna wake zenu? Si ndiyo maana mnaibiwa, kwanza nyie ndiyo mnasababisha maradhi aidha kwa wake zenu au kwa haohao mahawara zenu kwa sababu ya mchezo unaochezeka.

Sasa basi kilichonituma kuwaandikia si kuwakumbusha mnavyoibiwa tu bali kukemea hili kwa mahawara zenu na kwenu nyie kwani hili ni janga ambalo linawaingiza watoto wadogo wenye tamaa kwenye maambukizi ya magonjwa ya zinaa ambalo kwa asilimia kubwa linasababisha na penzi la vijana na watu wazima.

Mnaibiwaje?

Wasichana wengi wanapoingia kwenye uhusiano na wanaume watu wazima si kwamba wanakuwa wanawapenda kwa dhati bali wanatafuta hela zao na pembeni wanakuwa na mwanaume mdogo wa kuendana na yeye ambaye ndiye anampenda kwa dhati.

Kugharamia wawili

Mabinti wa aina hii huwagharimu sana wanaume wao watu wazima kwani hela wanazowapa huwagharimia na hao wapenzi wao kuanzia mavazi hadi maradhi.

Hivi mwanaume wewe unalijua hili? Ukiwa kwa mkeo usiku yeye analala na ampendaye imekuwa kama fasheni kwa sasa mwanamke kumiliki wanaume wawili anayempa matunzo kwa penzi la wakati na anayeishi naye kwa penzi la kudumu.

Sasa nimefafanua wanaume mnaibiwaje lakini niwarudie nyie mabinti mnaofanya hivyo, kwanza unahatarisha maisha yako kwani huenda siku moja akakufumania na kukukuta na kijana kisha akakuua kwa wivu.

Pili ni magonjwa ambayo mnaweza kuambukizana kwa kuwa na mzunguko wa mtu mmoja hili ni tatizo kubwa ambalo watu hawalioni kwani hata huyo kijana anaweza kuwa na mtu wake wa pembeni pia kwa kibinti anakuja kuchuna tu, sasa hesabu hapo unajikuta umejumuisha watu wanne walioko kwenye mzunguko wa penzi moja.

Vijana wenye tamaa nao ni tatizo kubwa siku hizi, hawapendi kufanya kazi na wapo tayari kuchangia penzi na mzee ili tu wapate pa kuishi na kula yao iwe nzuri,  siyo vizuri nawasihi wote wenye tabia hii kuacha mara moja.

Kama umetokea kumpenda mtu mzima basi mkubali alivyo na umuoneshe mapenzi ya kweli, kama unaona hakufai basi achana naye kabisa ili uwe na penzi lenye amani.

Hakuna kitu kibaya katika maisha kama usaliti hasa kwa mtu anayekupenda na kuamua kukusaidia kwani akijua unamchiti atakufanyia kitu kibaya ujute maishani.

Leave A Reply