The House of Favourite Newspapers

WANAWAKE KAENI CHONJO… MKE AUAWA KWA SUMU

DAR ES SALAAM: Mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Hajra Salehe, mkazi wa Magomeni Mwembechai jijini Dar amekutwa amefariki dunia chumbani kwake huku kukiwa na tofali pembeni yake na kitambaa kinachosadikiwa kuwa na sumu.  Tukio hilo lililowaliza wengi linadaiwa kutokea usiku wa Septemba 20, mwaka huu na kuacha maswali mengi hasa kuhusu mhusika wa mauaji hayo na sababu hasa za kufanya hivyo.

 

UNDANI WA TUKIO

Katika kupata undani wa tukio hilo, mwandishi wetu alifunga safari hadi nyumbani kwa marehemu na kufanikiwa kuonana na dada yake aitwaye Asha Salehe ambaye alieleza anachokifahamu kuhusu kifo cha mdogo wake huyo aliyeacha watoto wawili wadogo.

Alisema kuwa, siku ya tukio Hajra aliyekuwa anafanya kazi kwenye Duka la GSM, lililopo Lumumba Kariakoo alitoka kazini na kuwasiliana na baadhi ya ndugu zake akiwaeleza kuwa, alikuwa akielekea nyumbani kwake kupumzika.

 

“Wakati akifanya mawasiliano hayo hakuwa akijua kuwa kifo kipo mbele yake masikini, saa nne usiku alimpigia simu ndugu yetu mmoja na kumwambia alipanga aende kwake lakini hataweza kwa kuwa alihitaji kupumzika.

“Ilipofika saa 9 usiku, akamtumia rafiki yake sms akimwambia yuko na mzazi mwenzake aitwaye Ramadhani Idd ambaye kwa muda mrefu walikuwa wametengana. “Alivyomtumia ujumbe huo, rafiki yake akashangaa, akajiuliza saa tisa usiku inakuwaje yuko na huyo mzazi mwenzake? Hata hivyo alipuuza, akasema angemtafuta asubuhi.

 

“Asubuhi akawa anamtumia meseji, hajibu ndipo alipopiga mara kibao bila kupokelewa, machale yakamcheza na kuamua kwenda nyumbani kwake kwani siyo mbali sana, alipofika alishangaa kuona mlango uko wazi hivyo akapitiliza hadi ndani.

“Alipoingia ndani akamkuta Hajra amelala chini akionekana wazi amekufa, alishtuka sana na pembeni aliona tofali na kitambaa,” alidai dada huyo.

 

TAARIFA YASHTUA WENGI

Baada ya rafiki huyo wa marehemu kukuta hali hiyo, aliamua kutoa taarifa kwa ndugu, jamaa na marafiki ambao walifika na kushangaa kumuona Hajra amelala chini akiwa amekata roho.

“Simanzi ilitawala, hakuna aliyeamini kwamba Hajra alikuwa ametutoka, inauma sana. Wanaye wanasikitisha, wala hawajui kama mama yao ndiyo hawatamuona tena,” alisema ndugu huyo wa marehemu.

SUMU YAHUSISHWA

Baadhi ya ndugu wa marehemu ambao hawakutaka majina yao yaandikwe gazetini walisema kuwa, wanahisi Hajra ameuawa kwa sumu licha ya kwamba pia alikutwa na jereha usoni.

“Aliyefanya mauaji haya lazima atakuwa ametumia sumu, ni kweli marehemu alikutwa na jeraha lakini kile kitambaa kinaonesha kilikuwa na sumu, huenda walimpiga kisha wakammalizia na sumu,” alidai ndugu huyo.

Hata hivyo baada ya mauaji hayo kutokea, polisi walifika na kuuchukua mwili ambapo waliufanyia ‘postimotamu’ kabla ya kuukabidhi kwa ndugu ambao waliuzika Septemba 21 katika makaburi ya Kinondoni.

 

MASWALI KIBAO

Kifuatia tukio hilo, maswali mengi yameibuka kuhusu nani wanahusika na mauaji hayo, kwa nini wamemuua? Je, ni kweli siku hiyo marehemu alikutana na mzazi mwenzake huyo na walizungumza nini? Je, kuna uwezekano wa mume wake kuhusika?

Maswali hayo hakuna aliyeweza kuyapatia majibu licha ya madai kuwa, mpaka gazeti hili linakwenda mtamboni, mume wa marehemu hakuwa akifahamika aliko na kwamba kuna watu waliotiwa mbaroni wakihusishwa na tukio hilo.

POLISI WANASEMAJE?

Mwandishi wetu alifanya jitihada za kumtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, ACP Jumanne Muliro ambapo kila alipopigiwa simu hakupokea na baadaye akatuma ujumbe kwamba atafutwe baadaye.

 

WANAWAKE WAKAE CHONJO

Utafiti wa gazeti hili umebaini kuwepo kwa matukio ya wanawake wengi kuuawa kwenye mazingira ya kutatanisha hivyo wanatakiwa kuwa makini katika kila hatua ya maisha yao ili ikibidi kujiepusha na vifo hivyo.

Comments are closed.