The House of Favourite Newspapers

WANAWAKE WANAVYODUMISHA NDOA ZAO KWA NJIA HATARISHI !

NI wiki nyingine tulivu kabisa tunakutana kupitia safu hii ambapo tunazungumzia mada mbalimbali zinazogusa maisha yetu ya kimapenzi.  Namshukuru Mungu kwa uwezo alionipa wa kuandika mambo ambayo yamekuwa na msaada mkubwa katika maisha ya wengi. Niwashukuru pia wale ambao wamekuwa wakinipigia simu na kunitumia sms za kunipongeza kwa kile ambacho nimekuwa nikiwaandikia. Kabla ya kwenda mbali naomba niseme kwamba, tunatakiwa kuwapenda wale wanaoonesha mapenzi ya dhati kwetu. Kama uko ndani ya ndoa na umebahatika kumpata mtu sahihi ambaye anakupa furaha kila siku, nawe jitahidi kumfurahisha.

Kama uko kwenye uhusiano wa kawaida na mtu ambaye amekuwa akiufanya moyo wako uwe na amani, nawe chukua nafasi yako. Ndugu zangu, sehemu kubwa ya maisha yetu inatawaliwa na mapenzi. Ukijitahidi kuiweka sawa idara hiyo, mengine yatakwenda sawia lakini ikiwa mapenzi yatakutatiza, utakuwa ukishindwa kufanya mambo mengi ya msingi na hatimaye kujuta kwa nini umeletwa hapa ulimwenguni.

Lakini sasa, kuna jambo ambalo nimeona leo nilizungumzie hata kwa ufupi kutokana na nafasi finyu niliyotengewa. Kuna baadhi ya wanawake walioolewa ambao wamekuwa wakijiamini sana kwamba hawawezi kusalitiwa, ndoa zao haziwezi kuvunjika eti wakidai kuwa, wamewaweka waume zao viganjani.

Meneno haya yaweza kuwa si mageni masikioni mwako. Huenda ulishawahi kumsikia mwanamke akisema: ‘Mimi mume wangu hafurukuti kwangu, nimemuweka kiganjani na hawezi kunisaliti kwani nampa kila kitu’. Maneno haya yana tasfiri nyingi. Anayesema haya inawezekana kajidanganya kwa kwenda kwa waganga na kapewa vilimbwata vyake hivyo anaamini vitamfanya mumewe asimsaliti.

Mwingine anaweza kusema maneno hayo akimaanisha kuwa, anampa mumewe kila aina ya penzi, hata yale ambayo hayaruhusiwi (mfano mapenzi kinyume na maumbile) hivyo eti hakuna kitu ambacho anaweza kukifuata nje. Hii inatokana na ulimbukeni wa baadhi ya wanawake kuwa, eti wanaume wengi wanatoka nje ya ndoa zao kufuata kitu hicho.

Mwingine anaweza kusema hivyo akiwa na kitu kingine anachokitegemea, siyo mbaya lakini kinachoniuma ni kwamba asilimia kubwa ya wanawake wanaosema maneno hayo hawana sababu za msingi za kusimamia. Nataka kuwaambia wanawake kuwa, kujiamini ni kitu cha msingi sana kwenye ndoa lakini kujipa imani kuwa eti mumeo hawezi kukusaliti kwa kuwa unamuendea kwa mganga au unamruhusu ‘aruke ukuta’ ni kujidanganya.

Kujiamini kwako iwe ni kwa sababu unajua ‘kumhendo’ mumeo kwa kumpa mapenzi ya kiwango cha juu, kumheshimu, kumjali na kumpatiliza katika mambo ya msingi ambayo anastahili kuyapata kutoka kwako. Ukifanya hivyo utaifanya roho yake imsute kila anapotaka kukusaliti.

Hiyo ndiyo iwe sababu ya wewe kujiamini na wala huna sababu ya kujinadi kwa wenzako. Tambua kuwa kuna wanaofikia hatua ya kuhatarisha maisha yao kwa kutoa mapenzi kinyume na maumbile wakidhani eti ni njia ya kuwashika waume zao kumbe wanajitafutia matatizo makubwa.

Wapo waliopoteza fedha zao nyingi kwa kwenda kwa waganga ili waume zao wasifurukute mbele zao lakini imekuwa kazi bure. Shituka leo, anza kutumia mbinu sahihi za kuishikilia ndoa yako na usijidanganye kwa kufanya mambo ambayo ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu.

Mwanamke aliyekamilka ni yule anayeuthamini mwili wake, sasa kwa nini leo hii ukubali ‘kumrukisha ukuta’ mumeo eti ili kumfanya asiende nje? Kwa nini utumie fedha zako kwenye kumtafutia limbwata mumeo wakati wewe mwenyewe ni limbwata tosha? Ifike wakati tuyathamini maisha yetu hasa ya kimahusiano. Tatambue kuwa tuna kila sababu ya kuzitunza ndoa zetu kwa hali na mali lakini isiwe kwa njia ambazo ni hatarishi.

Yapo ambayo tunaweza tukatumia pesa na muda wetu mwingi kuyafanya ili kuwashika wapenzi wetu lakini ikawa ni kazi bure. Labda niwaambie tu kwamba, wengi ambao wamefanikiwa kudumisha ndoa zao wala hawajaenda kwa waganga na kupewa malimbwata, wao wenyewe wamegeuka malimbwata kwa kuwa wabunifu na watundu linapokuja suala la mapenzi. Wewe unakwama wapi? Tafakari na uchukue hatua sahihi!

Comments are closed.