The House of Favourite Newspapers

Wanawake wawili Kenya wabadilishana waume zao

 

WANAWAKE wawili kutoka kaunti ya Busia, magharibi mwa Kenya, wamewaacha watu na bumbuwazi mara baada ya kubadilishana waume zao kwa lengo la kutafuta furaha.

Lilian Weta mwenye umri wa 28, mama wa watoto watatu na Millicent Auma mwenye umri wa miaka 29, mwenye watoto wawili, wamezua gumzo katika mitandao nchini Kenya kwa kuonekana kuwa wamefanya jambo la ajabu sana kwa wanandoa hao kuamua kubadilishana wenza.

Wiki moja iliyopita wapenzi hao waliandikishiana serikalini namna ambavyo watoto watalindwa baada ya wanawake hao kubadilishana waume zao  na watoto.

Wanawake hao wanadai walifikia maamuzi hayo baada ya kusukumwa na ugomvi usioisha katika familia zao. Vyombo vya habari vya Kenya vimemripoti Lilian akisema alifikia uamuzi huo mara baada ya mume wake kumleta mwanamke mwingine katika nyumba yao mwezi mmoja uliopita.

“Mume wangu alinidanganya kuwa binamu yake kutoka Bungoma anakuja kututembelea, hivyo niandae chakula, na sehemu ya kulala mgeni.   Muda mfupi ulipita ambapo kuna mwanamke aliingia na kuniambia nimuachie nafasi kwa sababu hiyo ni nyumba yake la sivyo anidunge kisu,” Lilian alisema.

Lilian aliendelea kusimulia kuwa Auma alimwambia akamtafute mume wake na akimpata aoane naye,  na kweli alimtafuta mume wa Millecent na kwenda kufunga ndoa halali wiki tatu zilizopita.

“Mwanamke huyu alikuja akilia na kulalamika kuwa mke wangu amemchukua mume wake na nyumba yake.

“Nilimwambia kwamba kama mke wangu ndiye amekufukuza kwako basi nenda ukachukue mizigo yako na watoto na uje ukae na mimi hapa,” alisema Bwire ambaye alikuwa mume wa Millecent.

Ni wiki mbili sasa zimepita tangu Lilian Weta alipoolewa na Christopher Bwire baada ya wapenzi wao kuwasaliti na wanadai kuwa hawajutii kitendo walichokifanya.

Bwire ameviambia vyombo vya habari nchini humo jinsi maisha yake yalivyobadilika na kuwa ya furaha. “Wabaya wawili wapatane na wawili wazuri wapatane, sina msongo wa mawazo. Siku hizi ninaamka muda ninaotaka na kulala muda ninaotaka,  ninakula vizuri, nina furaha sana kuwa na Lilian,” alisema Bwire.

Na upande wake, Lilian pia anadai kuwa ana furaha sana kukaa na Bwire. Barasa ambaye ni mume wa zamani wa  Lilian anasema kuwa hana haja ya kumfuata mke wake na hataki kujua chochote kuhusu yeye kwa sababu yeye na Auma wana furaha sana.

Comments are closed.