
WAFANYABIASHARA wanne wa madini, Mohammed Innamula, Mubarack Mullas, Rivzi Yoonus (wote raia wa Sri Lanka) na Mtanzania mmoja, Mehboob Rattansi, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam kwa tuhuma za makosa mbalimbali ikiwemo kukutwa na madini mbalimbali yenye thamani ya zaidi ya Tsh milioni 42 pamoja na makosa ya utakatishaji fedha.

Akiwasomea mashtaka hayo, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Wankyo Simon, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi, Godfrey Issaya, amesema washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka sita ambayo wanadaiwa kutenda mnamo Januari 8, 2021, katika Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam wakisafirisha madini bila ya kuwa na leseni ya biashara hiyo.
Baada ya kuwasomea mashtaka hayo hakimu Isaya amesema kesi hiyo haina dhamana kwa kuwa miongoni mwa makosa yanayowakabili yamo ya utakatishaji fedha hivyo watuhumiwa watakaa rumande hadi itakapotajwa tena Januari 28 mwaka huu.

