The House of Favourite Newspapers

Wanyarwanda Wamfungua Akili Mkongo Yanga

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, amekiangalia kwa umakini kikosi chake jinsi kinavyomaliza michezo yao katika mechi tatu za mwisho kisha ameibuka na kuweka bayana kuwa, kuna kitu anakihitaji kukifanya ili timu hiyo iwe na makali zaidi tofauti na mambo yalivyo kwa sasa.

 

Kocha huyo raia wa DR Congo ameweka bayana kuwa licha ya kupata ushindi mara mbili kwenye mechi hizo tatu za mwisho za timu yake lakini kuna mambo hayaendi sawa kwa sababu ya kukata pumzi kwa wachezaji wake kiasi ambacho kinawapa nafasi wapinzani wao kufanya kile wanachokitaka.

 

Zahera ambaye ni kocha msaidizi wa timu ya taifa ya DR Congo, ameshtuka baada ya kipigo walichokipata kutoka kwa Rayon hivi karibuni.

 

Kocha huyo alizitaja mechi ambazo timu yake ‘pumzi ilikata’ kwenye dakika 15 za mwisho ni ule mchezo dhidi ya Waarabu USM Alger kisha mchezo wa Ligi Kuu Bara mbele ya Mtibwa Sugar na mechi dhidi ya Rayon Sport ya Rwanda. Mechi dhidi ya USM Alger na Mtibwa walishinda kwa mabao 2-1, dhidi ya Rayon walifungwa bao 1-0.

 

Kocha huyo ambaye kwa muda huu yupo na timu ya taifa ya Congo wakijiandaa na mchezo wa kufuzu Kombe la Mataifa Afrika (Afcon), ameliambia Championi Jumatatu kuwa kuna kitu ambacho anatakiwa akifanye ndani ya wachezaji wake ili waweze kumaliza muda huo wa dakika 15 za mwisho ambazo wachezaji wake wanakuwa wamechoka.

 

“Kwenye mechi za karibuni, tunashindwa kumaliza vizuri zile dakika 15 za mwisho na kuwaruhusu wapinzani wetu wafanye kile ambacho wanakitaka, hilo lilitokea kwa kiasi kikubwa kwenye mchezo wetu ule na Mtibwa ambao ilibaki kidogo wao waweze kupindua matokeo.

 

“Jambo zuri ni kwamba tumeliona mapema na tutalifanyia marekebisho kwa kiasi kikubwa ili pale ligi itakaporejea tena basi tuwe hatuna tatizo hilo ndani ya timu,” alisema Zahera ambaye ni miongoni mwa raia wa Congo wanne ambao wapo katika timu hiyo, wengine ni mshambuliaji Heritier Makambo, Papy Tshishimbi na kipa Klaus Kindoki.

 

Said Ally, Dar es Salaam

Comments are closed.