The House of Favourite Newspapers

Waoaji, waolewaji miyeyusho tupu-2

couplehappilysleepingNi Jumatatu nyingine murua, sina budi kumshukuru mwenyezi Mungu kwa kutukutanisha kwenye safu yetu hii nzuri ya mapenzi na uhusiano ya XXLove. Asanteni wasomaji kwa kutuma maoni na kupiga simu katika kuchangia mada ya ‘Waoaji, Waolewaji Miyeyusho Tupu’ ambayo tuliianza wiki iliyopita.

Wiki hii tunaendelea na sehemu ya pili ya mada hii kwa kusoma maoni ya baadhi ya wasomaji, lakini pia kutazama zaidi upande wa wanaume au waoaji.
Lengo la makala hii ni kuwazungumzia watu wa pande zote kwa maana ya mwanaume na mwanamke kwani bila ushirikiano wa watu hawa wawili basi hakuna uhusiano wa kimapenzi.

MSOMAJI
Binafsi napenda kuwasihi wasichana wenzangu, kujitambua na kujithamini sana hasa katika suala la uhusiano ili tusije tukaharibu maisha ya baadaye.

MSOMAJI
Nianze kwanza kwa kutoa pongezi kwenu kwa mada nzuri za kuelimisha jamii, wanaume na wanawake hawapendi kuolewa au kuoana kwa sababu ya usaliti ambao hufanywa na wanandoa walio wengi.

MSOMAJI
Upendo wa dhati umepungua, utakuta mke au mume wa mtu ameolewa au kuoa lakini mitaani michepuko kibao. Watu wengi kwa sasa wanalenga masilahi. Ukimtangazia mwanamke unataka kumuoa anakuuliza una kazi gani? Sasa kazi na kuoana vinahusiana nini?

MSOMAJI
Vijana wengi wa kiume wakitaka kuoa hawaangalii sifa muhimu, wengi huangalia sura na umbile zuri ambavyo si vitu vya msingi, mwisho wa siku ndoa hazichukui muda mrefu.

ZERISH WA CHAMAZI KWA MKONGO
Ndoa kwa sasa zimekuwa kama fasheni, unaolewa mwezi huu, unaachika mwezi ujao. Kwa sisi wasichana tunahitaji umakini wa hali ya juu sana katika utambuzi. Ukiamua kuolewa ni dhahiri umeamua kuachana na ukapera, unapaswa ufahamu mila, desturi na dini yako kama mama au baba wa familia.

MSOMAJI
Naomba ushauri, mimi ni binti, nina mchumba wangu, nifanyeje ili anioe kwani kila nikimwambia suala la kuoana anajifanya kama hasikii?
Ukweli huko hivi, wapo wanawake wanaotamani kupata mume wa kumuoa lakini wanaume au mume hapatikani, vivyo hivyo hata wanaume wapo wanaolia na kuomba kila siku ili wapate mke mwema wa kuoa lakini bado hawajapata.

Wanaume ni sababu kubwa sana ya wanawake kutokuolewa. Wengi wanapenda kuonja bila kujua nani atakayewaoa hao waliowaonja.

Ingawa wapo vijana wengine wanaosema kama maisha ni moja ya sababu ya wao kutokuoa, japokuwa wataalam wanasema maisha ndiyo hayohayo cha msingi ni makubaliano na kuanza kupigana na ugumu wa maisha. Ukisema unajipanga kwanza maisha yako yawe vizuri, basi utasubiri sana na utazeeka bila kuwa na familia.

Rekebisha mwenendo wako wa kila siku ili mwisho wa siku upate rehema ya kupata mwenza bora ambaye mtajenga familia makini na bora.

Tukutane wiki ijayo kwenye mada nyingine motomoto. Pia usikose kutembelea ukurasa wetu wa Mimi na Uhusiano kwenye Mtandao wa Facebook na Instagram kujifunza mengi kuhusu mapenzi.

Comments are closed.