visa

Waoo…! Kama Jana Vile!-11

ILIPOISHIA RISASI JUMATANO:

Baba Monica alikuja juu, alianza kuhisi kuchanganyikiwa. Alitambua kuna jambo baya kalifanya mkewe na mwanaume huyo…

“Hebu kaa hapa kwanza,” alisema baba Monica, mama Monica wakati anakaa akaangusha saa, viatu na zile pesa alizopewa na Magembe…

TAMBAA NAYO SASA…

“Haa! Haa! Mama Monica, hivyo vitu umevitoa wapi wewe?!”

Mama Monica alijisikia aibu, akabaki ametumbua macho asemeje! Kwamba amenunua? Kwa sababu gani? Maana kama ni viatu lazima viwe ndani ya bajeti, kama ni saa anayo, pesa za mauzo hazifikagi wingi ule hata kama angeuza chakula chote…

“Da! Magembe ananiponza hivihivi. Nitajibu nini mimi mtoto wa mzee Mashoka?”

“Si nakuuliza wewe mama Monica? Husikii au hutaki kunijibu?”

“Baba Monica siyo kwamba sitaki kukujibu, nakaa kwanza… hizi pesa, saa na viatu si vyangu. Ni vya mama Salama, si unamjua? Mchana alipita pale kwenye kibanda changu, akaacha, akasema atakuja kuchukua baadaye lakini kama nitaondoka hajafika nije navyo nyumbani. Atavifuata hapa,” alisema mama Monica huku akiangalia pembeni kwa aibu ya dhamira.

“Kwa hiyo atavifuata?” aliuliza baba Monica kwa sauti iliyojaa umakini…

“Ndiyo.”

“Sawa.”

***

Asubuhi ya saa moja, baba Monica alisimama nje kwake, akamwita mtoto wa jirani, akamtuma kwenda kumwita mama Salama…

“Mwambie anaitwa na mama Monica aje kuchukua vitu vyake.”

“Sawa.”

Mtoto akatoka mbio mpaka nyumbani kwa mama Salama…

“Hodi…”

“Karibu, ingia…kumbe Jumanne, hujambo?”

“Sijambo. Unaitwa na mama Monica, eti ukachukue vitu vyako.”

“Mimi? Vitu gani?”

“Sijui.”

“Sawa, mwambie nakuja,” alisema mama Salama huku kichwani akijiuliza ni vitu gani ambavyo aliviacha kwa mama Monica, alikosa jibu.

Baada ya dakika tano tu, akaondoka mpaka kwa mama Monica. Alimkuta baba Monica amekaa sebuleni. Alimkaribisha…

“Karibu sana mama Salama.”

“Asante sana.”

Mama Monica aliposikia sauti ya mama Salama alitoka mbio chumbani…

“Karibu mama Salama…”

“Asante…umefuata ile mizigo yako?”

“Eee.”

Mama Monica aliingia chumbani haraka sana.

Nyuma, mama Salama akawa bado anajiuliza kuhusu hiyo mizigo lakini akashindwa kumuuliza baba Monica kwani alivyojua yeye, aliyemuita ni mke wake, si mume…

“Au amechanganya majina? Pengine kapewa vitu vya mama Salama mwingine yeye akajua ni mama Salama mimi!” alijiuliza, pia akakosa majibu. Akabaki kusubiri tu.

Mama Monica alitoka, akamkabidhi vile vitu huku akimwambia…

“Karibu sana bwana, mimi ndiyo najiandaa kutoka kwenda kibaruani kwangu.”

Ilibidi mama Salama asimame ili kuondoka huku macho yake yakitua kwenye uso wa mama Monica kama ataambiwa lolote kwa ishara lakini wapi!

Baba Monica naye alisimama, akaongozana kumtoa mama Salama sambamba na mke wake…

“Haya baadaye,” alisema mama Salama…

“Haya, nisalimie vijana,” alisema mama Monica.

Waliporudi ndani, baba Monica akamwambia mke wake…

“Usalama wako ulikuwa hapo tu. Kama mama Salama asingekuja kuchukua mzigo wake, ningekukata masikio maana nina wasiwasi sana na huyo mwanaume unayesema anakutongoza kila siku.”

“Wala, mimi sina mpango naye hata kidogo. Kwanza wa nini? Au ni hizo pesa zake?”

“Kumbe ana pesa ee?” aliuliza baba Monica huku akimwangalia mkewe kwa macho yaliyojaa maswali kibao.

“Anavyodai.”

Mama Monica alijiandaa, akaondoka zake. Alitaka kupitia kwa mama Salama, lakini akajiuliza…

“Nitamwambia nini? Nikisema ni vitu vyangu nilihongwa na buzi langu ataniona mimi kumbe mchepukaji. Mbaya zaidi yeye ni mama mtu mzima na mimi ni mdogo kwake.

“Inabidi tu nihesabu potea. Siku nikikutana naye akiniuliza, nitamwambia kuna mtu alileta nimpelekee yeye.”

Ghafla mbele yake alitokea mama Salama akiwa amekunja sura ile mbaya mpaka mama Monica akaanza kuogopa …

Je, nini kiliendelea hapo? Usikose kusoma kwenye Gazeti la Risasi, Jumatano ijayo.

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!
Toa comment