The House of Favourite Newspapers

Waoo..! kama jana vile!-12

0

ILIPOISHIA RISASI JUMAMOSI:

“Nitamwambia nini? Nikisema ni vitu vyangu nilihongwa na buzi langu ataniona mimi kumbe mchepukaji. Mbaya zaidi yeye ni mama mtu mzima na mimi ni mdogo kwake.

“Inabidi tu nihesabu vimepotea. Siku nikikutana naye akiniuliza, nitamwambia kuna mtu alileta nimpelekee yeye.”

Ghafla mbele yake alitokea mama Salama akiwa amekunja sura ile mbaya mpaka mama Monica akaanza kuogopa …

JIACHIE MWENYEWE SASA…

 “Afadhali nimekuona mama Monica. Unajua sijui lolote kuhusu vile vitu nilivyokuja kuchukua nyumbani kwako!”

Palepale mama Monica naye akakumbuka kwamba, ilikuaje mama Salama akaenda kwake kuchukua vitu vyake wakati yeye hakumuita na alimdanganya tu mumewe…

“Kuna mtu alivileta kwenye biashara yangu, akasema nikuletee wewe…”

“Mh! Mwanaume, mwanamke?”

“Mwanamke. Alisema mpelekee mama Salama.”

“Alijitaja jina?”

“Hapana.”

“Mh! Haya, nitajua siku moja.”

“Halafu we ulijuaje kama nina vitu vyako mpaka ukaja asubuhi kwangu?”

“Si ulimtuma mtoto, yule nani sijui, Jumanne.”

“Jumanne! Mi sijamtuma mtu yeyote kwako.”

“Khaa! Basi Jumanne ndiyo aliyekuja kwangu, akasema unaitwa na mama Monica. Si ndiyo nikaja,” alisema mama Salama, mama Monica akashangaa sana.

Mara, akatokea Jumanne mwenyewe…

“Enhee! Si yule pale, we Jumanne,” aliita mama Salama…

“Naam.”

Jumanne alifika huku mama Monica akimkazia macho yenye maswali kibao…

“Unakumbuka ulikuja kwangu asubuhi?”

“Uliniambiaje?”

“Nilikwambia unaitwa na mama Monica ukachukue vitu vyako. Ukasema unakwenda.”

“We Jumanne, mimi leo tumeonana?” mama Monica aliuliza kwa kupandisha sauti kidogo. Hata mama Salama naye akaanza kushangaa kwamba, kama kweli Jumanne hakutumwa, sasa alijuaje kwamba mama Monica ana vitu vyake?

“Hatujaonana,” alijibu Jumanne.

“Sasa nani alikutuma?”

“Mi alinituma baba Monica, akasema nenda kwa mama Salama kamwambie kuna mzigo wake kwa mama Monica, ndiyo nikaenda kumwita.”

Mama Salama alielewa, lakini mama Monica alianza kuingia shaka kwamba, kumbe mumewe bado alikuwa kwenye upelelezi wa kujiridhisha kama kweli vitu vile ni vya mama Salama ndiyo maana akamtuma Jumanne kwa siri.

Basi, mama Monica aliagana na mama Salama akaenda kwenye biashara yake ya mamalishe.

Siku hiyo mpaka inafika saa tisa, Magembe alikuwa hajafika…

“Mh! Huyu leo vipi? Mbona hana dalili ya kuja, ana nini?” alijiuliza.

Saa kumi…

“Mh! Huyu si bure, lazima kuna kitu. Au anaumwa?”

Saa kumi na moja…

“Loo! Ngoja nimcheki kwenye simu.”

Mama Monica alimpigia simu Magembe, haikuwa hewani…

“He! Au amepoteza simu?” alijihoji mwenyewe mama Monica. Akaamini kuwa, lazima Magembe atakuwa amepata tatizo, tena kubwa ndiyo maana hakuwepo hewani.

“Hata kama kapoteza simu au kapata tatizo kubwa si angekuja kunifahamisha kuliko kuniweka roho juu,” mama Monica aliwaza.

Mama Monica akiwa amepoteza uchangamfu aliendelea kumuwaza Magembe na kukumbuka mambo aliyomfanyia na maneno yake matamu walipokutana kule gesti.

“Mama Monica, unajua siamini, siamini kama nipo na wewe kitandani?” mama Monica alikumbuka moja ya maneno ambayo Magembe alimwambia.

Mama huyo hakuishia hapo aliwaza namna Magembe alivyompeleka puta mpaka kijasho chembamba kikamtoka na jinsi kila mmoja alivyoishiwa nguvu na kujitupa huko baada ya kufika mwisho wa safari ya mahaba niue kwa pamoja.

“Inamaana huyu mwanaume hajanimisi kwa yote tuliyofanyiana na kuamua kuzima simu kabisa?” mama Monica aliendelea kuwaza.

Baada ya kuwaza sana, mama huyo aliamua kuendelea kuwajibika mara simu yake ikaita moyo ukapiga pa kwani alihisi mpigaji alikuwa Magembe.

Alipoitoa kifuani alipokuwa ameiweka na kuangalia mpigaji alikuwa mzoa taka, akatoa msonyo mkali uliosikiwa na wasichana wake wa kazi.

“Eh! Mama imekuwaje tena badala ya kupokea simu unasonya?” Tina Mapepe alimwuliza.

“Na wewe sitaki maswali yako ya kipolisi,” mama Monica alimjibu kwa mkato.

“Jamani mama yamekuwa hayo tena, kwani sisi wanao tukijua kilichokukera kuna tatizo gani?” Tina Mapepe alimwuliza.

“Tina, nimekwambia niache na mambo yangu sipendi unifuatefuate!” mama Monica alimwambia Tina.

Baada ya Tina kuambiwa hivyo alijua mama Monica hakuwa sawa, akawakonyeza wenzake waendelee na kazi.

Wakati mama Monica akizungumza na Tina Mapepe simu aliyopigiwa na mzoa taka iliita mpaka ikakatika mara ikapigwa tena.

Kwa hasira mama Monica aliikata na kuizima kabisa, akaenda kukaa kwenye kiti cha plastiki kilichokuwa karibu yake.

Siku iliisha bila Magembe kuonekana mpaka mama Monica anafika nyumbani kwake, hakuwa na mawasiliano. Alipopata nafasi alimtumia meseji Magembe lakini haikuonesha kama imefika kwenye simu ya mwanaume huyo.

“Au alitaka…” alitaka kumalizia mama Monica lakini akasita.

***

Kulikucha, siku ya pili. Mama Monica alipoamka kabla ya kufanya lolote aliangalia kwanza simu yake, kama meseji kwenda kwa Magembe ilifika, akakuta iko pembeni…

“Mh! Si bure,” alisema, akaanza kuingiwa na wasiwasi. Aliwaza mengi harakaharaka. Aliwaza kwamba, huenda Magembe ni mwathirika na ndiyo maana anasambaza ‘mahela’ ili kuwapata wanawake awaambukize na yeye.

“Huu ukimya wa Magembe una ujumbe ndani yake,” alisema moyoni huku akianza kupitia namna mwanaume huyo alivyomnasa kirahisi…

“Angekuwa mtu mzuri asingenizimia simu. Kama ana tatizo lolote lile angeniambia.”

Siku hiyo aliandaa chakula huku kila wakati akitupia macho kwenye simu yake akiamini anaweza kukuta meseji ya Magembe. Lakini wapi!

“Mh! Saa tano sasa, hajatuma meseji wala hajaniambia kitu. Ina maana hajapata meseji yangu au?” alijiuliza moyoni mama Monica huku akijisikia kukosa amani.

Wateja walianza kufika, saa sita na nusu hiyo. Lakini mpaka inafika saa nane, Magembe hakuwa ametokea…

“We Nina,” mama Monica alimuita msichana wake mmoja…

“Abee…”

“Hivi yule kaka aliyekuwa anakuja na pikipiki unamjua?” aliuliza mama Monica…

“Hapana dada, ila kuna siku alipoondoka kuna yule mteja wetu anayependa pilipili, alisema anamjua amefiwa na mkewe juzijuzi baada ya kuugua kwa muda mrefu…”

“Unasema?” mama Monica aliuliza kwa mshtuko.

Leave A Reply