Waoo…! Kama Jana Vile!-13

ILIPOISHIA RISASI JUMATANO:

“We Nina,” mama Monica alimuita msichana wake mmoja…

“Abee…”

“Hivi yule kaka aliyekuwa anakuja na pikipiki unamjua?” aliuliza mama Monica…

“Hapana dada, ila kuna siku alipoondoka kuna yule mteja wetu anayependa pilipili, alisema anamjua amefiwa na mkewe juzijuzi baada ya kuugua kwa muda mrefu…”

“Unasema?” mama Monica aliuliza kwa mshtuko.

TAMBAA NAYO SASA…

“Mimi ndiyo aliniambia hivyo yule mteja wa pilipili. Sasa sijui,” alijibu msichana huyo wa kazi bila kujua kuwa, kauli yake imemshtua sana mwanamke huyo…

“Kwa hiyo kumbe alifiwa na mke siyo?”

“Mimi niliambiwa na yule mteja wa pilipili.”

“Kwa nini hukuniambia sasa?”

“Ha! Kwani mi nilijua kama unamfahamu mke wake yule kaka. Mi sikujua.”

Mama Monica aligundua kuwa, msichana wake wa kazi hakujua yeye ana maana gani!

“Mh! Sasa huyo mwanamke alikufa kwa ugonjwa gani?” alijiuliza mama Monica akiwa amesimama huku amejishika kiuno kwa mshangao.

“Hiki kifo. Nadhani mke wake amefariki dunia kwa sababu ya ugonjwa wa Ukimwi! Kumbe ndiyo maana alikuwa ananimwagia minoti ili aninase aniambukize na mimi! Loo! Nakufa hivihivi najiona…tamaa mbaya kweli.”

Mama Monica alishika tena simu yake, akaseti namba za Magembe na kumpigia, akajibiwa ‘namba unayoipiga, haipatikani kwa sasa.’ Akatafadhalishwa kujaribu tena baadaye.

“Mh! Haya!” aliishia hivyo mwanamke huyo.

Muda wa chakula ulifika, wateja walianza kuwasili huku mama Monica akimtarajia zaidi Magembe.

Saa saba, Magembe hakutokea wala mtu mwenye pikipiki kama Magembe hakufika hapo achilia mbali kupita.

Ilikuwa saa nane na nusu, Magembe aliwasili akiwa ndani ya gari dogo jipya. Wakati analiegesha eneo hilo, mama Monica hakujua kama ni Magembe, ila alihisi ni mteja mwingine kabisa.

Alipomwona Magembe, mama Monica alishtuka sana. kwanza alikunja sura halafu akaikunjua kwa furaha ya mbali kwani alijua ataweza kumuuliza kuhusu kifo cha mkewe na pia atajua msimamo wake kuhusu mapenzi ambayo itategemea na majibu ya Magembe kuhusu kifo cha mkewe na ugonjwa uliomuua…

“Mambo  mama Monica?” alisalimia Magembe kwa sauti iliyojaa uzito wa uanaume…

“Poa, karibu mteja wangu. Umenikimbia.”

“Ah! Usijali, jana nilishinda bandarini.”

“Na simu ndiyo umezima?”

“Simu ilitumbukia kwenye maji juzi, basi sijaenda kuirudishia laini yangu. nataka namba zilezile.”

“Oke, karibu sana. Mi nikajua umeshasepa.”

“Hamna bwana,” alisema Magembe huku akikaa kwenye kiti chake kilekile anachokalia siku zote.

“Vipi, kama kawaida?” aliuliza mama Monica akiwa amemsogelea na kusimama mbele yake kwa adabu kubwa, maana si tayari mambo f’lani.

“Ndiyo mama Monica.”

Mama Monica alimuagiza msichana kumuandalia chakula Magembe, yeye akavuta kiti kingine na kukaa jirani na mteja wake huyo ambaye pia ni mpenzi wake.

“Hivi kwa nini ulizima simu Magembe?”

“Mama Monica si nimekwambia. Hukunielewa?”

“Ah! Sawa! Nina swali jingine Magembe…”

“Uliza mama Monica…”

“Kuna mtu alikuja hapa akasema anakufahamu, ulifiwa na mke hivi karibuni, ni kweli?”

“Ni kweli.”

“Alikuwa anaumwa nini?”

“Ajali! Kama ulisikia hivi karibuni kuna ajali ilitokea maeneo ya Kibamba…”

“Ndiyo nilisikia.”

“Basi na yeye alikuwepo.”

Mama Monica aliyekuwa akiongea na Magembe huku amemsogelea karibu kabisa, alirudi kwa nyuma na kuegemea kiti kisha akavuta pumzi kwa kasi…

“Kwani huyo mtu alisema mke wangu alikufaje?”

“Eti aliugua kwa muda mrefu sana,” alisema mama Monica huku akimwangalia usoni Magembe kuona atajibu nini…

“Ha! Huyo hanifahamu hata kidogo. Mke wangu alikufa kwa ajali,”Magembe alisema akitoa simu ya smart phone na kumwonesha mwanamke huyo picha za ajali ya gari…

“Unaona?”

“Ee ndiyo, pole sana baby,” mama Monica alichombezea na jina la mapenzi.

“Asante mpenzi wangu.”

Baadhi ya wateja walisikia mazungumzo ya mama Monica na Magembe, wakashangaa kugundua kuwa, kumbe mwanamke huyo jamaa yake wa mchepuko ni huyo.

Mara aliingia yule mteja anayependa pilipili, wasichana wa kazi wakamwangalia mama Monica ambaye naye alimwona mteja huyo akiingia…

“Mapilipili karibu sana.”

Je, nini kiliendelea hapo? Usikose kusoma kwenye Gazeti la Risasi, Jumatano ijayo.

Loading...

Toa comment