Waoo…! Kama Jana Vile!-17
ILIPOISHIA RISASI JUMATANO:
“Mh! Atakuwa nani? Ni mama Monica au kaka yake, Daudi? Maana sina namba ya Daudi lakini kama ni mama Monica kwa nini atumie namba nyingine?” alijiuliza kisha akaipokea simu hiyo kwa ujasiri mkubwa…
“Haloo…”
JIACHIE MWENYEWE…
“Haloo,”alipokea Magembe.
“Haloo bwana Magembe, mimi Daudi, kaka yake mama Monica uliyekuwa naye gesti na pia ni rafiki yako wa siku nyingi…”
“Ee! Niambie mkubwa…”
“Hivi ni kweli ulikuwa unakutana na dada yangu na kinga? Maana yeye nimemuuliza amesema hujawahi kutumia kinga kwake hata siku moja…”
“Amekudanganya bwana Daudi. Mimi siwezi kumfanyia ukatili huo mwanamke. Mdogo wako labda amejichanganya kusema hivyo.”
Daudi alikata simu, akaiweka pembeni kwa kuitupa. Magembe kwake ilikuwa kama siku imeharibika, kwani alipomaliza kuzungumza na Daudi bado akawa na mawazo juu ya meseji ya mama Monica…
“Lakini kweli, akisema aende kwa wanasheria atanifunga. Maana itaonekana naambukiza wanawake Virusi vya Ukimwi kwa makusudi.”
Aliwaza sana Magembe, mwisho wa yote akaamua kumtumia meseji mama Monica…
“Please, naweza kukutana na wewe hata kwa dakika kumi tu?”
“Unataka kuniambia nini?”
“Tukikutana nitakwambia mpenzi wangu.”
Mama Monica alifikiria kwa muda, akajiuliza anaitiwa nini, akaamua kukubali…
“Poa, wapi? Lakini sasa hivi…”
“Ee sasa hivi…mimi ndiyo natoka hapa, tukutane pale kwenye baa yetu.”
“Sawa.”
***
Magembe ndiye aliyetangulia kufika kwenye baa hiyo, akakaa na kuagiza bia ya kwanza ya baridi. Mara, akaingia mama Monica. Alivaa kinyumbani kama si ki mamamama…
“Za saa hizi?” alisalimia mama Monica huku akivuta kiti na kukaa…
“Poapoa,” alijibu Magembe kwa sauti ya haraka huku sura yake ikikaza chini kwa aibu.
Mhudumu alifika akamsikiliza mama Monica, naye akaagiza bia ya baridi.
Walianza kunywa, tena polepole huku mama Monica akionekana mwenye shauku ya kutaka kujua alichoitiwa…
“Vipi nyumbani? Hawajambo?” aliuliza Magembe kwa sauti nzito sana tofauti na siku nyingine…
“Hawajambo kabisa, sijui kwenu?”
“Kwetu kuko poa…eee nimetaka tukutane ili tuweke mambo sawasawa.”
“Sawa nakusikiliza,” alisema mama Monica huku akivuta kiti mbele ili kukaa sawasawa.
“Ulinitumia meseji kwamba nimekutana na kaka yako kwa hiyo nimekuambukiza Ukimwi, utanifunga…kwani yeye ndiyo amekwambia tulikutana?”
“Hajaniambia mlikutana, ila ameniambia amejua mimi nilikuwa na wewe.”
“Oke. Je, amekwambia mimi nina Ukimwi?”
“Ndiyo…akaniuliza kama tulikuwa tunatumia zana, nikamwambia tumekuwa tukitumia.”
“Si umemwambia hatukuwa tunatumia!”
“Nimemwambia tulikuwa tunatumia.”
Kwa mbali Magembe alijihisi unafuu moyoni kusikia kuwa, mama Monica alimdanganya kaka yake kuhusu kutumia kinga…
“Sasa sikia mama Monica…mimi sina Ukimwi kama watu wanavyosema, ila tabia za watu ndiyo hizo. Si ajabu mtaani kwenu kuna watu wanasema wewe una Ukimwi. Iko hivyo…
“Hata kazini kwetu, kuna bosi wangu mmoja watu wanasema ana Ukimwi, lakini tangu wameanza kusema huu ni mwaka wa kumi sasa, jamaa yupo na ana afya njema. Mkewe mzima, watoto wazima…
“Nashangaa sana, mimi mke wangu kufa kwa ajali wanasema ni Ukimwi. Sasa je, angekufa kwa kifua kikuu wangesemaje?”
Mama Monica alibaki amemtumbulia macho Magembe na sera zake hizo. Akili yake ilikuwa nusu kwa nusu. Kwamba ni kweli mwanaume huyo hana Ukimwi na pia ni kweli anao…
“Umemaliza?” aliuliza mama Monica baada ya Magembe kukaa kimya kwa dakika moja nzima…
“Nimemaliza, labda kama wewe una ujumbe wowote…”
“Mimi ujumbe wangu si wewe huna Ukimwi?” aliuliza mama Monica…
“Ndiyo sina…”
“Tukapime wote hata kesho.”
“Sawa, mimi niko tayari,” alisema Magembe huku kichwani akijua ukweli. Lakini pia alijua mama Monica akicheza naye vibaya anaweza kumfunga kweli kama siyo kumwaibisha kabisa hata kwenye vyombo vya habari.
“Kwa hiyo kesho tunakwenda kupima siyo?”
“Nimesema niko tayari, kesho tukapime.”
“Saa ngapi na tutakutana wapi?” aliuliza mama Monica.
“Tukutane Hospitali ya Palestina, saa saba mchana.”
“Sawa, mimi nitafika pale saa tano na nusu.”
“Utakuwa umewahi sana mama Monica.”
“Si vibaya.”
“Oke. Lakini mimi nina ombi langu mama Monica.”
“Lipi?”
“Basi kabla hatujaachana twende gesti tena kidogo.”
Je, nini kiliendelea hapo? Usikose kusoma kwenye Gazeti la Risasi, Jumatano ijayo.