The House of Favourite Newspapers

Waoo..! kama jana vile!-18

0

ILIPOISHIA RISASI JUMAMOSI:

Ilikuwa bahati mbaya sana kwani wakati Magembe anatoka kwa kujichungachunga, kaka wa mama Monica naye akawa anatoka sijui kwa ajili ya kwenda wapi!  Wakakutana macho…

“Ha! Magembe…”

“Ha! Daudi…”

TAMBAA NAYO MWENYEWE…

Kila mmoja alimshangaa mwenzake kwa kumwona pale gesti. Lakini kaka wa mama Monica alishangaa zaidi kwani alijua kwamba, dada yake alikuwa akimpa uroda mwanaume huyo lakini nyuma ya pazia ya Magembe ndiyo kulikuwa na tatizo kubwa…

“Magembe wewe ndiyo umelala na dada yangu mama Monica?” aliuliza Daudi…

“He! Kwani mama Monica ni dada yako?”

“Sasa je? Lakini bwana Magembe lengo lako nini kuniulia dada ‘angu?! We unajua afya yako ilivyo…kweli umeamua kumwambukiza Ukimwi wako hivihivi?”

“Noo! Bwana Daudi huwa natumia kinga, kwani si najijua!”

“Una uhakika?”

“Nina hakika.”

“Nikimuuliza ataniambia hivyo?”

“Labda aamue kusema uongo,” alijibu Magembe kwa sauti iliyojaa aibu na dhamira mbaya.

Daudi alirudi ndani, akafikia kujitupa kitandani na kujishika kichwa huku machozi yakimchuruzika. Demu aliyekuwa naye akamuuliza…

“Vipi tena baby? Mbona umerudi na mawazo halafu kama ulikuwa unaongea kwa sauti hapo nje wakati simu ipo ndani. Ulikuwa unaongea na nani?”

“Ah! Kuna jamaa amenikera sana.”

“Jamaa gani baby?”

“Ah! Kuna mjinga mmoja hivi, n’takwambia siku nyingine.”

***

Magembe alitembea kuelekea kwenye gari huku akiwa na mawazo kibao. Aliwaza jinsi alivyoumbuka na Daudi…

“Kama kweli mama Monica ni dada yake ina maana atamwambia siri zangu. Mama Monica atajua mimi ninaishi na virusi. Lakini sidhani…anaweza kweli kumuuliza dada yake kama mimi natumia kinga ninapokutana naye? Akiweza atakuwa jasiri sana maana ni aibu kwa tamaduni zetu,” alisema moyoni Magembe.

***

Mama Monica alipofika kwake, alimpigia simu Magembe ili kumwambia alifika salama…

“Lo! Sawa baby…na mimi ndiyo nafika,” Magembe alijibu hivyo, akikwepa kumwambia ukweli kwamba alikutana na kaka yake. Lakini hilo mama Monica mwenyewe alilikumbuka, akamuuliza…

“Hivi baby, ulipotoka hujaonana na kaka yangu kweli?”

“Hapana, sijaonana na mtu yeyote yule,” Magembe alijibu haraka sana.

“Afadhali,” alijibu mama Monica.

Nusu saa mbele, mama Monica simu yake iliita. Akaangalia kwenye kioo na kubaini ni kaka yake…

“He! Kuna nini tena?” alijiuliza moyoni akiichukua ili kuipokea…

“Za saa hizi kaka…”

“Njema…hivi wewe mama Monica, yule Magembe unamjua vizuri au unamjua juujuu tu?”

“Namjua kaka…”

“Ni nani wako?”

“Kaka samahani sana, niliteleza mdogo wako…naomba unisamehe sana…”

“Ni mara ngapi umeshakutana naye?”

“Mara mbili tu.”

“Mlitumia kinga?”

Swali hilo liliufanya moyo wa mama Monica kulipuka lip! Ukaanza kwenda kwa kasi…

“Ndiyo kaka Daudi…”

“Una uhakika? Maana yule bwana anaishi na virusi vya Ukimwi.”

Ghafla simu ya mama Monica haikuwa hewani, alianguka na kupoteza fahamu.

Baada ya nusu saa alizinduka na kukuta amezungukwa na mwanaye Monica na msichana wake wa kazi…

“Pole mama,” msichana wa kazi alimwambia. Monica alikuwa akilia tu…

“Asante…simu yangu iko wapi?” aliuliza mama Monica. Msichana wa kazi akamwonesha ilipo. Ni palepale alipoangukia.

Mama Monica aliichukua simu hiyo, akasoma meseji ilivyoingia. Ni ya kaka yake, Daudi…

“Naona simu yako imakata ghafla. Pole sana kama ni chaji. Kama kweli mlitumia kinga sawa. Lakini kama hamkutumia, nenda kapime. Yule bwana mke wake alikufa kwa ngoma na watu wanasema yeye ndiye aliyemwambukiza mkewe ngoma.”

Mama Monica akaenda chumbani kwake na kumwaga machozi tena huko…

“Kumbe Magembe alionana na kaka Daudi! Mbona mimi amenikatalia hawakuonana? Au kaka Daudi alimwona lakini Magembe hajamwona?” alijiuliza mama Monica huku akifuta machozi kwa shuka.

Alijikausha sana macho ili arudi katika hali yake ya kawaida mumewe asije akamkuta kwenye sura yenye utata.

Mama Monica alijiuliza maswali mengi sana kuhusu Magembe lakini mwisho wa yote alikubali moyoni kwamba, mwanaume huyo alifanya makusudi kutembea naye ili amwambukize Ukimwi…

“Nitakwenda kupima. Kama kweli nitakuwa nimepata maambukizi lazima nimfungulie mashtaka Magembe,” alisema moyoni mama Monica huku akijitahidi kuzuia machozi yasimtoke.

Alijikaza sana, akamtumia meseji Magembe…

“Kumbe ulikutana na kaka yangu ukanidanganya. Nashukuru sana kwa kuamua kuniua kwa makusudi. Ila lazima nitakufunga Magembe.”

Magembe alipopata ujumbe huo alijikuta akiweweseka. Akakaa kwanza juu ya kitanda chake na kuinamisha kichwa.

Mara simu yake ikaita, namba haijui…

“Mh! Atakuwa nani? Ni mama Monica au kaka yake, Daudi? Maana sina namba ya Daudi lakini kama ni mama Monica kwa nini atumie namba nyingine?” alijiuliza kisha akaipokea simu hiyo kwa ujasiri mkubwa…

“Haloo…”

 Je, nini kiliendelea hapo? Usikose kusoma kwenye Gazeti la Risasi, Jumamosi ijayo.

Leave A Reply