The House of Favourite Newspapers

Waoo..! kama jana vile!-24

0

ILIPOISHIA RISASI JUMAMOSI:

“Sasa sikia, mimi kesho asubuhi nitadamkia nyumbani kwa baba Salama. Nitampa maelezo yote ya vitu na fedha za mke wake kupitia kwa wewe, ili nione kama anajua haya mambo au mke wake ana siri moyoni…”

“Mh! Baba Monica, ndiyo nini sasa?” aliuliza mama Monica huku akikaa kwenye kitanda.

JIACHIE MWENYEWE…

“Kwani wewe unataka kumkingia kifua mama Salama au?”

“Sikingi kifua baba Monica, ila nadhani sasa unataka kutibua ndoa ya watu. Je, kama zile pesa anazipata kwa njia haramu, huoni kama utakuwa umevunja ndoa ya watu?” alihoji mama Monica kwa sauti iliyojaa utulivu.

“Haiwezekani awe anapata pesa kwa njia haramu halafu maisha yenyewe yawe vile. Kwa nini asizitumie kwa kuboresha maisha yao? Au anajenga mahali kwa siri bila mumewe kujua?” alisema sana baba Monica.

Tafsiri ya haraka ya mama Monica ni kwamba, mume wake ameshtukia kuwa, vile vitu na pesa ni vya kwake ndiyo maana anataka kwenda kwa baba Salama ili aweze kupata uhakika…

“Hapa nikimwomba sana atashtukia. Lakini pia sitakiwi kumwacha aende. Na kwa hali hii, nikisema nimuwahi mama Salama asubuhi pia ni tatizo, naye atataka kuweka amani kwenye ndoa yake, anaweza akazikana pesa kama mume wangu atakwenda kwa mume wake,” mama Monica alisema moyoni mwake huku kiroho kikimdunda…

“Halafu ujue baba Monica mama Salama ni kama mama kwangu. Sasa ukienda kwa mumewe halafu mambo yakaharibika, atajua mimi ndiyo nimekwambia wewe kila kitu. Mimi nakusihi usiende. Tuwaache wao na maisha yao na sisi tuendelee na  maisha yetu,” mama Monica alijitahidi kuondoa msimamo wa mumewe kuhusu kudamkia kwa baba Salama.

Hata hivyo, baba Monica hakuzungumza tena na mke wake, alilala. Lakini kwa mama Monica, usiku huo haukuwa mzuri kwake. Usingizi ulikata, akahisi kama asubuhi inayofuata hali itakuwa mbaya sana kwake.

“Sasa nitakuwa nashughulika na mambo mangapi? Kuna hili, lakini kuna lile la kuhusu kupima virusi vya Ukimwi kesho. Vyote hivyo ni mimi tu! Da! Safari hii kweli nimepatikana. Lakini ni mimi mwenyewe nimejiingiza kwenye janga hili,” aliwaza mwanamke huyo.

***

Ilikuwa asubuhi ya saa kumi na moja, mama Monica alitoka kitandani akiwa hana hata lepe la usingizi…

“Da! Ama kweli usiku wa deni haukawii kukucha. Yaani mara hii kumekucha? Ina maana sijalala…?”

Alikwenda nje, akachukua fagio na kuanza kufagia wakati si kawaida yake yeye kufanya hivyo zaidi ya msichana wake wa kazi, Biligita.

Baba Monica alitoka kitandani, akaenda chooni. Baada ya kutoka huko, aliingia bafuni kuoga na kurudi chumbani kujiandaa.

Mama Monica kuona vile, alimfuata mumewe chumbani na kujaribu kuchunguza kwa alivyoweza yeye kama bado ana mpango wa kwenda kwa baba Salama…

“Mbona leo unawahi kutoka, kazini kuna mambo mengi?” aliuliza mama Monica lakini moyoni alitaka kusikia jibu la mumewe ili ajue mwelekeo…

“Kuna wageni watakuja asubuhi hii…lazima niwahi.”

‘Hunywi chai?”

“Chai mpaka baadaye, nitanywea kazini. Lakini pia napitia kwanza kwa baba Salama ndiyo maana nimetoka asubuhi sana,” alisema baba Monica na kuyafanya ‘matumbo’ ya mkewe kuunguruma kama mtu aliyepigwa na baridi kali akiwa hana nguo.

“Hivi baba Monica, bado una huo mpango mume wangu? Mimi nilidhani umenielewa?”

“Sijakuelewa chochote. Mpango ninao na ndiyo naondoka,” alisema baba Monica akitoka kwa hasira…

“Loo! Mambo yameharibika. Lazima mama Salama atajitetea kwa kusema fedha si zake, ni zangu. Sasa itakuaje?” aliwaza moyoni mama Monica.

Alitamani kumuwahi mumewe kwa baba Salama, kwamba aanze kufika yeye kabla ya mume wake.

Hapo, mawazo kwamba ana ahadi ya kwenda kupima Ukimwi na Magembe aliyaweka pembeni kwanza. Akasimamia hoja moja tu ya kutatua la mama na baba Salama.

Alikwenda kuoga, alipotoka akajiandaa haraka na kuondoka zake kwenda kwenye biashara yake lakini asubuhi hiyo alipitia njia inayopita nje ya nyumba ya mama Salama.

Alipita jirani kabisa na dirisha ili kama atasikia chochote kutoka ndani ya nyumba hiyo…

“Mimi nakwambia mama Salama…hili suala lazima ulitolee maelezo ya kina. Siamini hata kidogo kwamba, wewe unaweza kufanya kitendo kama hicho,” sauti ya baba Salama ilisikika katika mtindo wa kufoka.

Mama Monica alisimama sambamba na ukuta, akazidi kutega masikio…

“Baba Salama wala usipate shida. Ukweli ni huu nitakaokwambia mimi sasa hivi…”

“Upi?”

“Ni kwamba, pesa zote pamoja na hivyo vitu ni vya mke wake mwenyewe, mama Monica. Sasa sijajua kwa nini aseme ni mimi…lakini ngoja niwasilimulie kisa cha tangu siku ya kwanza kabisa,” mama Salama alifloo.

Mama Monica kule nje, dirishani ilibaki kidogo tu ajichafue kwa haja, maana hakuwa na uwezo wa kujizuia wala kujipa maelekezo ya kichwani.

Swali lake lilikuwa moja, maelezo hayo aliyokuwa akiyatoa mama Salama, je mume wake yupo sebuleni au la? Maana hakusikia sauti yake tangu yeye afike kwenye dirisha hilo…

“Kwa hiyo mimi nikawa sijui lolote. Lakini nikasema huenda vile vitu na pesa za mwanzo, ni mtu kakosea. Kwa hiyo niliviweka nikijua kuna siku mwenyewe halali atajitokeza na kumfuata mama Monica ambaye naye atanifuata mimi…

“Sasa jana usiku tena aliposema kuna pesa zangu, nikajua ni yaleyale. Ubaya ni kwamba nikifika pale, namwona shemeji mwenyewe baba Monica kama hayupo sawa. Halafu mama Monica yeye anakuwa na uso wa wasiwasi. Kwa hiyo nashindwa kuuliza kwa undani, nikijua kuna siku nitajua,” alisikika mama Salama huku akisimama…

“Sasa unasimama kwenda wapi?” aliuliza baba Salama.

“Nakwenda kuchukua vile vitu na pesa zake za awali ili ujue sijatumia hata kitu kimoja kama nilivyokwambia.”

Mama Monica alitaka kuanguka, akazidi kujibanza ukutani. Alitaka sana kujua kama mume wake yupo au la! Alitegemea kitendo cha mama Salama kusimama kwenda chumbani, huku nyuma, mume wake na baba Salama lazima wangeongea…

“Itakuwa baba Monica ameyabwaga mambo halafu yeye kaenda zake kazini,” aliwaza mama Monica ambapo kwake aliona ni afadhali mambo yake yanavyomwagwa bila mumewe kujua kuliko akiwepo. Alipanga moyoni kuingia kwenye nyumba hiyo na kuwaangukia ili yote yaliyosemwa na mama Salama yasifike kwa baba Monica…

“Unajua baba Monica, hawa wanawake bwana wanataka ufuatiliaji kama huu ulioufanya wewe,” baba Salama alisikika akimwambia baba Monica…

Je, unajua nini kiliendelea hapo? Usikose kusoma kwenye Gazeti la Risasi, Jumamosi ijayo.

Leave A Reply