The House of Favourite Newspapers

‘Wapambe’ Wa Riek Machar Wakamatwa Sudan Kusini

Vikosi vya Sudan Kusini vimemkamata Waziri wa Mafuta na maafisa kadhaa wakuu wa kijeshi waitifaki wa Makamu wa Kwanza wa Rais, Riek Machar; huku wanajeshi wakiendele kuizingira nyumba yake katika mji mkuu, Juba.

Naibu Mkuu wa Jeshi, Jenerali Gabriel Duop Lam, mpambe wa Machar, alikamatwa siku ya Jumanne, huku Waziri wa Mafuta, Puot Kang Chol akikamatwa jana Jumatano pamoja na walinzi wake na jamaa zake.

Hakuna sababu iliyotolewa ya kukamatwa kwa watu hao; kamatakamata ambayo imekuja baada ya kundi lenye silaha linaloshirikiana na Machar kuteka kambi ya jeshi katika jimbo la Upper Nile, kaskazini mwa nchi hiyo.

Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Februari, upinzani nchini humo ulishutumu vikali hatua ya kulipuliwa kwa kambi yake moja ya kijeshi na jeshi la Sudan Kusini, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Picha za helikopta ya kijeshi zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii, zilionesha “mashambulizi ya mabomu” katika Kaunti ya Ulang huko Upper Nile.

Msemaji wa upinzani alisema katika taarifa kuwa vituo vya mkutano vya vikosi vya upinzani vilishambuliwa kwa mabomu na jeshi la serikali. Hali ya wasiwasi inaongezeka tena nchini Sudan Kusini licha ya wito wa kuheshimiwa makubaliano ya amani.
Chini ya mkataba huo uliotiwa saini mwaka wa 2018, serikali ya umoja wa kitaifa na mpito iko mjini Juba.