The House of Favourite Newspapers

Wapenzi waliogombana, tiba ni hii hapa

 KUGOMBANA ni jambo ambalo halikwepeki katika uhusiano wa kimapenzi. Upo ugomvi ambao ni wa kawaida na huisha kirahisi lakini upo ugomvi ambao huwa mkubwa na kama ukitokea na ukashindwa kujua nini cha kufanya ili kuweka mambo sawa, husababisha ufa kwenye penzi lenu.

Leo nitazungumzia mambo muhimu ya kufanya inapotokea wewe na mpenzi wako mmeingia katika ugomvi, mmetoleana maneno machafu au hata kupigana. Kwanza, tafakari chanzo cha tatizo. Kuna usemi kwamba ukitaka kulitatua vizuri tatizo ni lazima kwanza ujue chanzo cha tatizo lenyewe. Ukishindwa kugundua chanzo cha tatizo, basi na wewe unakuwa sehemu ya tatizo.

Utashangaa kwamba wapenzi wengi hugombana na mambo kuwa makubwa kabisa kwa sababu ya vyanzo vidogo ambavyo walishindwa kuvigundua mapema na matokeo yake vikazaa matatizo mengine. Mfano rahisi, chanzo kinaweza kuwa mpenzi wako amekupigia simu lakini ukashindwa kuipokea kwa muda muafaka. Atakapopiga kwa mara nyingine au mkikutana, usitegemee atakufurahia kwa sababu atahisi umemdharau kwa kutopokea simu yake.

Endapo utafanya makosa ya kushindwa kuliona kosa lako mapema na kushindwa kuomba radhi au kutoa maelezo yanayoeleweka kwa nini hukupokea simu, matokeo yake utamjibu vibaya, naye atakujibu vibaya na mwisho mtaishia kupigana au kuachana kabisa mkiwa mmeshatoka kabisa kwenye kosa la msingi. Bila shaka msomaji wangu umeona jinsi chanzo kidogo kinavyoweza kusababisha tatizo kuwa kubwa. Ndoa nyingi au uhusiano unaofika mwisho huwa umesababishwa na mambo madogo ambayo yalishindwa kutafutiwa suluhu mapema.

Katika kila ugomvi unaotokea, jambo la kwanza jipe muda wa kutafakari chanzo kilichosababisha mkagombana. Wakati mwingine wewe ndiye unaweza kuwa chanzo cha tatizo lakini kama ukiyajua makosa yako mapema na kukiri kisha kuomba radhi kwa mwenzio, utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kurudisha mapenzi kwa haraka.

Pili, mpe muda ili hasira zake ziishe. Kila binadamu ameumbwa akiwa na hasira na kwa bahati mbaya ni wachache wanaoweza kuzidhibiti hasira zao. Ni rahisi mtu kutukana, kupiga au kuharibu vitu akiwa na hasira.

Baada ya kugombana, kila mmoja lazima atakuwa na hasira na njia pekee inayoweza kuepusha matatizo zaidi, ni kujipa muda na kumpa muda mwenzako ili hasira zipungue. Tatu, mpe nafasi ya kutoa lililo moyoni mwake. Huwezi kumuelewa mtu kabla hujampa nafasi ya kuzungumza na kumaliza kile alichokusudia kukisema. Endapo tatizo limetokea na upo kwenye hatua za kusaka suluhu, mpe mwenzako nafasi ya kueleza dukuduku lililopo ndani ya moyo wake.

Usimkatishe wala kumbishia chochote, muache aongee ulichomuudhi mpaka dukuduku lake liishe kisha na wewe jieleze kwa upole na sauti tulivu. Nne, ni busara zaidi kuomba msamaha. Hakuna silaha nzuri inayoweza kukusaidia kuushinda ugomvi wowote na kutuliza mambo kabla hayajawa mabaya kama kuomba msamaha. Neno ‘samahani’ ni dogo lakini lina maana kubwa kwa yule mtu anayelitoa na anayelipokea.

Hata kama unaona dhahiri kwamba kosa siyo lako, omba msamaha kwanza kisha baada ya hapo anza kumuelewesha mpenzi wako kwa upole. Lazima mwisho na yeye atayaona makosa yake na kukuomba msamaha, mtaweza kuepuka kuukuza ugomvi huo na kurudisha hisia za mapenzi.

Ni hayo tu kwa leo, tukutane tena wiki ijayo.

Comments are closed.