The House of Favourite Newspapers

Wapo waliotambulishwa, wakaachwa Sembuse wewe!

0

blackcouple-bedsmileSHUKRANI na sifa ziende kwa Maanani kwa kunipa nafasi nyingine ya kukutana nawe msomaji wangu Jumanne hii. Ukiachia mbali changamoto  na matukio mbalimbali ambayo tunakutana nayo kila siku kikubwa ni kushukuru Mungu kwa kila jambo na kutokata tamaa.

Mada ya leo nitazungumzia watu ambao wanadhani wakitambulishwa na wapenzi wao kwa wazazi au familia zao basi inakuwa ni kifungo kwa mtu aliyemtambulisha kwa maana ya kujipa uhakika wa kuolewa au kuoa, wakati ukweli unaweza usiwe hivyo.

Suala la wapenzi kutambulishana katika familia za pande zote mbili ni sehemu ya utamaduni wa jamii kubwa ya Kiafrika ni jambo jema sana. Ila kuna kitu kikubwa sana cha kujifunza kwa baadhi ya wanaume na hata wanawake, nianze na wanawake.

Wanawake

Unaweza ukapata mchumba ambaye akapanga mipango yote kwa kuanza kukutambulisha kwa baadhi ya ndugu zake ambao yeye anaivana au anaelewana nao sana na wewe mwanamke ukaona kama umeshamkamata kwa kila kitu, kwani baadhi ya dada au kaka zake wanakufahamu na kukuita wifi au shemeji na wakati mwingine hata shangazi. Wakati huo mwanaume mwingine anaweza kufanya taratibu zote za kuja kwenu kujitambulisha kwa utambulisho feki ili kukuaminisha lakini mwisho wa siku akawa hana dhamira ya dhati ya kutaka kukuoa zaidi ya kutaka faragha na wewe tu!

Wanaume

Mara nyingi baadhi ya wanaume wengi wamekuwa wakilalamikiwa kuwa ni sehemu ya kuzalisha matatizo yanayosababishwa na uhusiano lakini ukweli ni kwamba wapo wanaume wengine ambo na wao walishawahi kuwatambulisha wapenzi wao wa kike kwa familia zao lakini mwisho wa siku wakaambuli manyoya kwa maana ya kuachwa na wapenzi waliowatambulisha.

Hali ikoje?

Wanaume na wanawake wengi wamekuwa wakilalamikiana au wakilizwa na mapenzi kila kukicha huku kila upande ukielekezea shutuma kwa upande mwingine, wanawake wanawaona wanaume kama watu wasiofaa katika uhusiano, kwani wanasema ni watu wenye tamaa. Vivyo hivyo kwa wanaume wengi wamekuwa wakiwalalamikia wanawake kuwa ni watu wasioridhika hata kama watafanyiwa kila kitu.

Ushuhuda

Mrembo mmoja aliwahi kupata bwana na akaonesha msimamo mzuri wa kumwambia jamaa kama anampenda kwa dhati na ana malengo naye ya kuwa mke wake wa ndoa basi wakatambulishane, kijana alikubali wakapanga siku na muda wa kufanya huo utambulisho, siku ilipowadia mwanadada akatambulishwa lakini mwisho wa siku aliyeolewa ni mtu mwingine, inaumiza na ilimuuma sana binti yule, kwanza ukiangalia umri wake alikuwa bado binti mdogo na ni kama jamaa alichezea maisha yake.

Hitimisho

Kila mtu anapaswa kuwa na hofu ya Mungu anapaswa pia amuonee huruma mwenziye ni kwa namna gani ataumia pindi atakapomdanganya kuwa anamuoa au kuolewa naye wakati moyoni mwake anajua kabisa kuwa hana mpango huo.

Leave A Reply