The House of Favourite Newspapers

Warembo wanaowabana wanaume kimataifa!

MIAKA ya nyuma kidogo ilikuwa ni vigumu kidogo kuona wasanii wa kike wakivuka mipaka ya nchi zaidi wasanii wa kiume, ndiyo waliokuwa wakithubutu.

Lakini kadiri muda unavyozidi kwenda, tunawaona mabinti kutoka kwenye Bongo Fleva; Vanessa Mdee, Nandy, Linah, Maua Sama ambao wameonekana wakijaribu kupambana na wasanii wa kiume kama vile Kiba, Mondi, Harmo, Rayvanny, Jux na wengine wengi ambao tayari wameshate-ngeneza majina yao kimataifa zaidi.

Kwa upande wa muziki unaofanywa na wadada hapa Bongo, una changamoto kubwa sana kutokana na wasanii wa kike kuwa wengi sana ndani ya Afrika ambao kwenye nchi zao kuna urahisi mkubwa wa kupata kolabo na wasanii wa nje na soko lao la muziki ni kubwa ukilinganisha na la hapa kwetu.

Mfano mzuri ni wasanii wa kike kutoka Nigeria am-bao wame-kuwa na urahisi mku-bwa hata ku-pata lebo nje na Afrika kama ilivyowahi kutokea kwa msanii Tiwa Savage baada ya kula donge nono kwenye lebo ya msanii Jay-Z iitwayo Rock Nation tofauti na hapa kwetu, aliyewahi kupata shavu ni Rosa Ree ambaye alipata dili huko Sauz ambapo alisaini mkataba na kuwa chini ya moja ya lebo kubwa Afrika, lakini mpaka sasa haifahamiki nini kinaendelea maana yuko nchini kwa kipindi kirefu wakati alipatiwa na makazi ya thamani kubwa huko Bondeni.

Kibongobongo, kuna baadhi ya wasanii wa kike wamethubutu na kufanikiwa kupiga shoo kimataifa au kushirikiana na wasanii wa kutoka nje ya Tanzania.

Hebu tuwatazame baadhi ya wasanii hao ambao wameonesha kuwakazia msuli wasanii wa kiume katika suala la kimataifa;

VANESSA MDEE

Vanessa Mdee maarufu kama Vee Money ni moja kati ya wadada wanaoipeperusha vizuri bendera ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo amefanya kazi nyingi sana ambazo zimeenda Kimataifa kama vile Nobody But Me aliyoshirikiana na msanii kutoka Afrika Kusini anayekwenda kwa jina la K.O, Kisela ambayo ameshirikiana na Kundi la Muziki la Destruction Boys la Afrika Kusini na nyingine nyingi ambazo amefanya na wakali tofautitofauti.

NANDY

Mwanadada huyu kwa sasa anakimbiza vibaya kutokana na kazi zake anazofanya huku akijichanganya kwenye aina mbalimbali za muziki kwani amekuwa akifanya kolabo nyingi kutoka kwa wasanii kutokea nchini Kenya kama vile Willy Pol na kundi la Muziki la Sauti Sol ambao ndiyo walikuwa majaji kwenye shindano kubwa la kusaka vipaji la Tusker, ambapo katika kipindi hicho Nandy alipata nafasi ya kushiriki, hivyo ilikuwa ndoto yake kubwa kuja kufanya nao kazi watu hao.

Usisahau kuwa Nandy ni miongoni mwa wasanii wa kike watatu kutoka Bongo walioweza kupata shavu la kupiga shoo kubwa juzikati pande za Dubai, inayokwenda kwa jina la One Music Africa Fest, shoo ambayo ilikuwa na miamba mikubwa ya burudani kutoka Afrika.

Kwa Nandy hii si mara yake ya kwanza, amewahi pia kufanya shoo hiyo mwaka jana.

LINAH

Linah kama ilivyo kwa Nandy, alianza muziki chini ya usimamizi wa Jumba la Vipaji Tanzania, Tanzania House of Talent (THT) ambalo lilimkuza na linaendelea kukuza vipaji mbalimbali Bongo.

Linah kwa kipindi kirefu kidogo alikuwa kimya, lakini kwa sasa amerejea na anafanya vizuri na ngoma zake mbili alizoziachia hivi karibuni, mojawapo iitwayo Same Boy akiwa ameshirikiana na mwanadada Recho na nyingine inayokwenda kwa jina la Koleza ambayo imeweza kukaa kwenye chati nyingi za muziki Afrika mashariki bila kushuka kwa kipindi cha miezi miwili.

Hiyo imetosha kabisa kuwa miongoni mwa wasanii walioipeperusha bendera ya Tanzania kwenye shoo ya One Music Africa Fest iliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita pande za Dubai.

ROSA REE

Ni mwenyeji wa Mkoa wa Kilimanjaro, hivi karibuni ameingia kwenye msala na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) baada ya video yake ya muziki ambayo inaonyesha sehemu kubwa ya maungo ya mwili wake kuwa wazi, ambayo ni kinyume na maadili ya Tanzania, lakini Rosa Ree ni mmoja kati ya wanawake ambao wanaisogeza gemu ya muziki wetu wa Tanzania mbali Kimataifa kutokana na kujituma pamoja na kazi zao kukubalika hasa nje ya Tanzania, jambo ambalo linasaidia kuuweka kwenye ramani ya dunia muziki wa Bongo Fleva kutokana na kufanya kolabo zake baadhi ambazo amezifanya kipindi cha nyuma na zikamfanya akae kwenye ramani nzuri ya muziki, kolabo hizo ni kama ile aliyofanya na mkali kutoka Sauz anayekwenda kwa jina la EMTEE ngoma iitwayo Way Up.

Ukiachilia mbali ngoma hiyo, pia ana ngoma kadhaa ambazo amezifanya na mkali kutoka nchini Kenya ambaye ni mpenzi wake anayefahamika kwa jina la Timmy Tdat

MAKALA:AMMAR MASIMBA

Comments are closed.