The House of Favourite Newspapers

WASAFI VS KONDE GANG… kamwe namba hazidanganyi

0

KWENYE maisha ya sasa, unapaswa kuogopa vitu vitatu; Mungu, teknolojia na muda. Fanya ufanyavyo, vitu hivi vitatu huwezi kuvikwepa maishani mwako. Chunga sana!  Ndani ya miezi mitano ya mwanzo wa mwaka 2020, kumekuwa na vita kali kati ya lebo kubwa mbili za muziki huu wa Bongo Fleva. Lebo hizi zimekuwa zikisikika zaidi katika kutoa kazi kali na bandika bandua.

Hapa nazungumzia Wasafi Classic Baby (WCB) inayomilikiwa na mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na Konde Gang Music Worldwide inayomilikiwa na mwanamuziki Rajabu Abdul ‘Harmonize’.  Wasafi ni lebo yenye jeshi kubwa kuanzia wasanii hadi viongozi, na Konde Gang ni jeshi linalosimama na mtu mmoja, japo nyuma yake kuna viongozi.

Makala haya ya OVER ZE WEEKEND yanakuletea video kali zilizotoka kati ya Januari na Mei, mwaka huu kutoka Wasafi na Konde Gang.

JANUARI

Ngoma za Wasafi ni Ate ya Mbosso ambayo hadi sasa ina watazamaji milioni 2.5. Nyingine ni Lavie ya Mbosso na Tanasha yenye watazamaji milioni 9.6, Tekenya ya Lava Lava ina watazamaji 2.3, Zipo ya Rayvanny ina watazamaji milioni 1.3, jumla zimekusanya watazamaji milioni 15.7 tangu zimetoka.

Kwa upande wa Konde Gang, Harmonize au Harmo alishiriki kolabo moja ambayo ni Remix ya Olver Twist akiwa na Skales na Falz, wote kutoka Nigeria ambayo imetazamwa mara laki 6.

FEBRUARI

Ngoma za Wasafi zilizotoka ni Jeje ya Diamond au Mondi yenye watazamaji milioni 18 hadi sasa. Nyingine zilizotoka Februari ni Gere ya Mondi na Tanasha yenye watazamaji milioni 13, Mama la Mama ya Rayvanny yenye watazamaji milioni 2.7, Teamo ya Rayvanny yenye watazamaji milioni 9.9, Vumilia ya Rayvanny yenye watazamaji milioni 1.4, Wanga ya Lava Lava na Meja Kunta, yenye watazamaji milioni 3.2, jumla ya idadi ya watazamaji kwa ngoma zote za Wasafi zilizotoka mwezi Februari ni milioni 48.2 hadi sasa.

Kwa upande wa Konde Gang, ziliruka ngoma kama Hujanikomoa ya Harmo yenye watazamaji milioni 2.1, Hainistui ya Harmo yenye watazamaji milioni 1.9 ambapo jumla ya watazamaji ni milioni 4 kwa ngoma hizo za  mwezi Februari.

MACHI

Wasafi iliachia ngoma kama Tamba ya Mbosso yenye watazamaji milioni 4.3, Corona ya Rayvanny yenye watazamaji milioni 2.4, Ex Boyfriend ya Rayvanny yenye watazamaji milioni 3, Miss Buza yenye watazamaji milioni 4, jumla ya ngoma zote zina watazamaji milioni 13.7 hadi sasa.

Kwa upande wa Konde Gang, ngoma zilizoruka mwezi Machi ni Mama ya Harmo yenye watazamaji milioni 1.6, Bed Room yenye watazamaji milioni 2.7, jumla ngoma zote zimekusanya watazamaji milioni 4.3 hadi sasa.

APRILI

kwa upande wa Wasafi, ngoma za mwezi Aprili ni Wana ya Zuchu yenye watazamaji milioni 3.4, Kwaru ya Zuchu yenye watazamaji milioni 2, Mauzauza ya Zuchu yenye watazamaji laki 3, Hakuna Kulala ya Zuchu yenye watazamaji laki 8, Watuone ya Zuchu na Mondi yenye watazamaji laki 3, Bachela ya Queen Darleen na Lava Lava yenye watazamaji milioni 1.4, jumla ya ngoma zote za Wasafi kwa mwezi Aprili, zimekusanya watazamaji milioni 18 hadi sasa.

Kwa upande wa Konde Gang, ngoma zilizotoka Aprili ni Bed Room Remix ya Harmo ambayo ina watazamaji milioni 1, Sawa ya Ibraah ambaye ni msanii mpya wa lebo hiyo, imetazamwa mara laki 4, Nimekubali ya Ibraah, imetazamwa mara laki 7, jumla ngoma hizo za Konde Gang zilitazamwa mara milioni 2.1 hadi sasa.

Konde Worldwide's New Artist Ibraah Set to Hold Virtual Concert ...

MEI

Ngoma za Wasafi zilizotoka mwezi Mei ni pamoja na Quarantine ya kruu nzima ya Wasafi yenye watazamaji milioni 2.4, Nisamehe ya Zuchu yenye watazamaji milioni 1 na Raha ya Zuchu yenye watazamaji laki 9. Jumla video zao kwa mwezi Mei zina watazamaji milioni 3.9 hadi sasa.

Kwa upande wa Konde Gang, ngoma zilizotoka mwezi Mei ni One Night Stand ya Ibraah na Harmo yenye watazamaji milioni 2.7 na Fall In Love ya Harmo yenye watazamaji laki 9. Jumla video zao zina watazamaji milioni 2.6 hadi sasa. Hadi hapo, nadhani utakuwa umeshapata jibu kuwa ni jeshi lipi linaonesha dalili ya kuishinda vita hii kwani hesabu hazidanganyi kutokana na kazi kali zilizotoka kwenye lebo hizo ambazo zimekuwa na ushindani mkubwa.

Leave A Reply