Wasafirishaji Wa Vifurushi Na Vipeto Nyanda Za Juu Kusini Watakiwa Kuwa Na Leseni
Wasafirishaji wote wa vifurushi na vipeto wanaofanya kazi katika kanda ya nyanda za juu kusini yametakiwa kutumia muda huu wa upendeleo kurasimisha huduma zao za usafirishaji kwa kuchukua leseni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Akizungumza katika mkutano wa wadau wa huduma za Kiposta Mkoa wa Mbeya Meneja wa TCRA kanda ya Nyanda za Juu Kusini Mhandisi Asajile John amesema umiliki wa leseni ya TCRA unaongeza mapato kwa watoa huduma kwani wateja wengi wanavutiwa zaidi kutuma mzigo kwa watoa huduma rasmi na kuondoa usumbufu namna ya upatikanaji wakati anahitaji kutuma kifurushi/Kipeto.
Amesema kuongezeka kwa wateja kunapelekea kuongezeka kwa mapato ya watoa huduma ambayo yanachangia ongezeko la pato la taifa.
Mhandisi Asajile amesema ili kufanikisha hilo TCRA imeanzisha mfumo wa utoaji leseni mtandaoni ujulikanao kama mfumo wa Tanzanite ambapo mtoa huduma anaweza kuomba hadi kupata leseni kwa njia ya mtandao jambo ambalo linarahisisha utendaji na kuokoa gharama.
Ameongeza kuwa iwapo waombaji hao wa leseni watakumbana na changamoto katika kuombq leseni wanaweza wasiliana na TCRA kupitia namba ya dawati la huduma ambayo ni 0800008272 au kufika katika ofisi yoyote ya Mamlaka kwa msaada zaidi.
Mkutano huu ni sehemu ya kampeni ya kuhamasisha wananchi kutumia huduma za watoa huduma wa kusafirisha vifurushi waliosajiliwa ijulikanayo kama TUMA CHAP kwa usalama ambapo inahusisha kuhamasisha watoa huduma wajisajili na jamii kuwatumia watoa huduma rasmi.