The House of Favourite Newspapers

Wasakwa kwa Kuchana Quran

0

WATU kadhaa wanaotuhumiwa kuchana kitabu kitukufu cha Dini ya Kiislam, (Quran) hadharani katika maeneo ya Pandani-Mtemani Mkoa wa Kaskazini-Pemba wanasakwa ili sheria ifuate mkondo wake.

Akithibitisha habari hizo, Afisa mmoja wa Polisi alisema watuhumiwa hao wanasakwa kwa udi na uvumba kwa sababu ya kusababisha uvunjifu wa amani.

“Wanaotuhumiwa kuchana kitabu hicho ni anayejulikana kwa jina moja la Bwana Eddy kutoka Tanzania Bara na Fatma Nassour wa Zanzibar,” alisema afisa huyo aliyeomba jina lake kuhifadhiwa kwa kuwa siyo msemaji.

Mwaka juzi mtumishi wa Serikali Wilaya ya Kilosa, Daniel Elimrigi, alifanya kitendo hicho ambacho kilizua sintofahamu na kuzua vurugu kubwa miongoni mwa jumuiya ya Dini ya Kiislam.

Kitendo cha kuchana Quran kiliibua hisia kali mongoni mwa waumini wa Kiislam nchini kwa kuwa Tanzania inaheshimu uhuru wa kuabudu hivyo kitendo cha kilichofanywa na watu hao kuchana kitabu hicho hadharani ni ukiukwaji mkubwa wa maadili ya Kitanzania.

Rais John Pombe Magufuli enzi za utawala wake aliwahi kutoa kauli kali ya kuwatafuta wahusika waliochana vitabu vitakatifu na kumfukuza kazi mfanyakazi wa Halmashauri ya Kilosa mkoani Morogoro, Daniel Elimringi ambaye alichana kitabu kitakatifu cha Quran hadharani na kurekodiwa katika video fupi iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii.

Huko nyuma Zanzibar iliwahi kukumbwa na migogoro ya kidini na kisiasa hali iliyosababisha baadhi ya wananchi kukimbilia uhamishoni mwaka 2001 na kuwa wakimbizi.

Machafuko hayo ya kihistoria yalisababisha watu wengi kufariki dunia na nyumba za ibada kuchomwa moto.

Ushahidi unaonesha kwamba kuanzia mwaka 2005-2016 makanisa mengi yalichomwa moto na kusababisha migogoro huko Zanzibar.

Katika tukio lingine, miaka kadhaa iliyopita, mtoto mmoja alifikishwa mahakamani kwa kudaiwa kukojolea Quran jambo lililoibua vurugu kubwa maeneo ya Mbagala jijini Dar.

Kama hiyo haitoshi, miaka kadhaa iliyopita, mtu mmoja Mkazi wa Nsemulwa Kichangani mjini Mpanda Mkoa wa Katavi, Jafeti Nobeti (15) alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Chiganga Ntengwe kwa tuhuma za kukojolea Quran Tukufu na sheria kuchukua mkondo wake.

STORI; WAANDISHI WETU, DAR

Leave A Reply