The House of Favourite Newspapers

Wasanii Kuchangiwa Fedha za Matibabu… Mchawi ni Nani?

HAINA ubishi kwamba tasnia ya Bongo Fleva na Bongo Movies zinaongozwa kwa kupendwa nchini kuliko tasnia nyingine. Kwanza zina mashabiki wengi, zinafuatiliwa kwa ukaribu na ndiyo maana hata zikitokea kuteleza sehemu f’lan serikali kupitia wizara husika hutoa tamko la onyo ama kufungia kile walichokikosea.

 

Lakini ukiachilia mbali kupendwa huko, ukija katika maisha ya mastaa wanaokubalika katika tasnia hizi wengi wao wanaishi maisha ya kati. Kwa miaka ya hivi karibuni kumekuwa na wimbi kubwa la wasanii hawa kupatwa na matatizo na mwisho wa siku kupitishwa harambee ya kupata fedha za kuwatibia nje ya nchi.

 

Swali la kujiuliza mchawi ni nani? Ikumbukwe wanatoka katika tasnia kubwa pengine kwa kiasi wanachoomba pindi wapatapo tatizo wangeweza kupatiwa matibabu bila kufanyiwa harambee. Katika makala haya, nachambua tu baadhi ya sababu zinazoweza kuchangia wasanii hawa kufikia hatua hiyo;

Usimamizi wa kazi

Tumekuwa tukiona kazi nyingi za wasanii wakubwa huku tukiamini mafanikio yao lazima yatakuwa juu. Ukweli wa yote, wasanii wengi kazi zao zinasimamiwa na kuendeshwa na watu wengine (makampuni/ mtu binafsi). Unakuta msanii anafanya kazi nyingi lakini asilimia kubwa anayenufaika ni kampuni au mtu binafsi anayemsimamia huku yeye akiambulia kiduchu.

KUJISAHAU

Haina ubishi kuwa wasanii wengi Bongo wanaofanikiwa hujisahau na kipindi akipatwa na matatizo anakuwa hana kitu hivyo wadau kulazimika kupitisha harambee ya matibabu. Ukiongelea filamu, wapo wanaochukua kuanzia milioni 10 kwa filamu moja na msanii huyo kwa mwaka anaweza kutengeneza filamu tatu hadi tano.

KUFEKI MAISHA

Inaweza kuwa sababu mojawapo, wasanii wengi Bongo wanaishi maisha ya kuigiza. Kuna ambao maisha yao ya kuungaunga na wapo ambao angalau. Ukiingia katika mitandao mingi ya kijamii wasanii hawa wanavyoanika maisha yao ni tofauti na uhalisia. Majumba, mitoko na baadhi ya magari siyo wanayomiliki bali kujionesha kwa jamii kuwa ana hadhi f’lan.

Kudhulumiwa/ kipato kiduchu

Hili limekuwa likiongelewa na wasanii wengi pindi wanapopatwa na matatizo. Wamekuwa wakilalamika kupata maslahi madogo au kipato kiduchu hivyo kwa muda wote walikuwa wakigangaganga njaa ilimradi wapate chochote waweze kuishi.

 

Wengi wao wameshindwa kujisimamia na wengine wanaishia kufungua ofisi za kujisimamia kazi zao na kuzifunga kutokana na kushindwa kuziendesha. Haijaanza leo Pengine jambo hili lingeweza kupatiwa suluhisho mapema leo hii wasanii wengi wasingekuwa wakiomba msaada wa matibabu.

Ikumbukwe kuwa, mwaka 2011 aliyekuwa muigazi wa filamu Bongo, Juma Kilowoko ‘Sajuki’ (marehemu) alikuwa na uvimbe pembeni ya ini na baada ya hapo ilipitishwa harambee ya wadau mbalimbali kumchangia na kufanikiwa kupata zaidi ya milioni 16 za matibabu katika Hospitali ya Apolo nchini India.

Msanii mwingine ni wa Bongo Fleva anayefanya Dancehall ambaye pia ni Prodyuza, Dolphin Pose ‘Jetman’. Jet alikuwa akiomba msaada wa kwa ajili ya kufanyiwa matibabu nchini India baada ya kupooza kutokana na maradhi ya uti wa mgongo kwa zaidi ya miaka mitano.

Redio, mitandao na magazeti mbalimbali yaliungana katika kufanya harambee ya kuchangiwa kwa msanii huyu ambapo ilikuwa ikihitajika kiasi cha shilingi milioni 12.

 

Baada ya Jet, mwishoni mwa mwaka jana msanii mwingine kutoka Bongo Movie, Ahmed Albaity ikabainika naye alikuwa akiteseka kwa zaidi ya miaka 10 akisumbuliwa na tatizo la uti wa mgongo baada ya kuanguka na kuvunjika shingo alipokuwa akiogelea ambapo kwa sindano moja pekee ilikuwa inagharimu dola za Marekani 26,000 (sawa na Sh.milioni 59 za Kibongo).

Hata hivyo, baada ya kuanza kwa harambee za kuchangishana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alikutana na msanii huyo na kutoa tiketi za ndege za watu wanne kwa ajili ya safari ya matibabu nchini China kwenye Hospitali ya Beijing ambapo alitibiwa na juzi amerejea nchini.

 

Msanii wa Bongo Movie, Wastara Juma ni miongoni mwa wasanii waliokuwa wakihitaji msaada wa matibabu nje ya nchi. Ikumbukwe kuwa, Wastara amekuwa akitembelea mguu wa bandia kwa zaidi ya miaka minne baada ya kupata ajali ya pikipiki iliyomsababisha kukatwa mguu.

Wastara alitakiwa kurudi India kwa matibabu na hakuwa na fedha hivyo ilimfanya apate maumivu ya mgongo na wakati mwingine kuzimia huku akilazimika kunywa dawa za maumivu mara kwa mara.

Kupitia mitandao ya kijamii, Wastara aliomba msaada kwa viongozi, mashabiki na watu wote kumpatia kiasi cha shilingi milioni 37 kutibiwa nchini India.

Wakati Wastara akifanikiwa kupata fedha za matibabu na kwenda kutibiwa kisha kurudi, mkongwe mwingine kutoka Bongo Movie, Amri Athuman ‘King Majuto’ naye yupo hospitali akiomba msaada wa matibabu ya nyonga.

Majuto ambaye ni lejendari wa vichekesho Bongo, amekuwa akisumbuliwa na nyonga kwa muda mrefu ambapo kwa sasa anatibiwa katika Hospitali ya Tumaini, jijini Dar.

Hivi karibuni wasanii wa Bongo Movie wakiongozwa na Steven Nyerere walisema kuwa wamesaidiwa tiketi mbili za matibabu nchini India kutoka Kampuni ya ASAS hivyo wanawaomba Watanzania wajitokeze kumsaidia gharama za matibabu.

Comments are closed.