The House of Favourite Newspapers
gunners X

WASANII Wakali wa Komedi Waliyochipukia

KAMA ulikuwa unajua Rowan Atkinson ‘Mr Bean’ ndiye mchekeshaji namba moja duniani, basi ulikuwa unajidanganya sana kwani yupo Charles Spencer Chaplin ‘Charlie Chaplin’ ambaye kutokana na kipaji cha kuchekesha alichokuwa nacho baadhi ya watu wanasema hajatokea kama yeye mpaka sasa kwenye Sayari ya Dunia hii!

 

Charlie, licha ya kuwa na umbo dogo, alikuwa akijua namna ya kumfanya mtu acheke, kuanzia kutembea kwake hadi visa! Alibuni mtindo wake wa uvaaji uliokuwa ukimtambulisha kuanzia kofia ya bakuli, mustachi, kifimbo na suti ya aina yake.

Charlie alifariki dunia mwaka 1977 akiwa na umri wa miaka 88, lakini hadi leo ameweka kumbukumbu katika vichwa na macho ya mashabiki kila wanapoona vipande vya video zake za vichekesho.

 

Kama ilivyokuwa kwa Charlie, vijana wengi Bongo wamekuwa wakifanya komedi ya visa vifupifupi vya kumfanya mtu abaki midomo wazi. Tumeona wengi wakitengeneza filamu zao na wengine vipande vifupi na kuvitupia katika mitandao ya kijamii.

Katika makala haya, tunakuletea baadhi ya wasanii wa vichekesho ambao ukipata nafasi ya kuangalia kazi zao utakubaliana na mimi kuwa wanaitendea haki kwa kile wanachokifanya kupitia usanii huo, lakini wengi wao wameibuka hivi karibuni na wameweza kujipatia majina kwa haraka;

SAIMBA MTINGITA (TABU MTIGITA)

Tabu amejizolea umaarufu mkubwa kupitia Mtandao wa Kijamii wa Instagram. Hii ni kutokana na anavyoigiza lafudhi ya Kimakonde (kutoka Mtwara), kitu ambacho kimemfanya kutengeneza mashabiki wengi na pia kumpatia matangazo ya biashara kupitia kazi yake hiyo.

ANNASTAZIA EXAVERY (EBITOKE)

Kama ilivyokuwa kwa Tabu katika kutumia lafudhi ya Kimakonde, Ebitoke naye amejizolea umaarufu kupitia lafudhi ya Kihaya pamoja na alama aliyojiwekea ya kujipaka wanja mkubwa na mweusi.

Ebitoke alianza kubamba kupitia Instagram pamoja na Youtube kipindi hicho akiwa chini ya Kampuni ya Timamu ambapo vichekesho vyake vingi alikuwa akishirikiana na wakali wengine waliokuwa wakichipukia kama vile Mjeshi na Mkali Wenu.

Kupitia kuchekesha huko, kulimfanya kutengeneza matangazo mengi ya kibiashara ya michezo ya kubahatisha.

MARTIN WHITE ‘TIN WHITE’

Mwigizaji huyu ni kaka wa mwanamuziki wa Bongo Fleva, Richard Martin ‘Rich Mavoko’, lakini ana kipaji kikubwa sana cha uchekeshaji na kama ukipata nafasi ya kuangalia vichekesho vyake, kamwe huwezi kuacha kuviangalia kila wakati.

Kwa wale wanaosafiri mikoani na mabasi, asilimia kubwa watakuwa walishavunjwa mbavu na Tin ambaye amekuwa akifanya filamu fupifupi akiwa sambamba na wachekeshaji wengine ambao ni Ringo na Kipupwe.

DULLVAN

Kama umepata bahati ya kuangalia vipande vyake akiigiza, unaweza kunikubalia kuwa ni mwigizaji anayechipukia, lakini amekubalika kwa haraka sana na umaarufu wa mchekeshaji huyu ameupata kupitia Mtandao wa Kijamii wa Instagram.

Dullvan amejipatia umaarufu kutokana na staili yake ya kuigiza akiwa katika muonekano mara tatu kwa wakati mmoja. Kama ilivyokuwa kwa wengine, naye vichekesho vyake vimempa madili kibao pamoja na kuwa balozi wa benki nchini.

JAYMONDY

Unaweza kusema ni pacha ya Dullvan kutokana na aina za uchekeshaji wao wa kufanya muonekano mara tatu kwa mtu mmoja, japokuwa mara nyingine amekuwa akichekesha kwa kutunisha pua yake au kubandika sura yake kwenye picha ya staa kutokana na tukio ‘linalo-trend’.

Jaymond amekuwa ni kipenzi cha wasanii wengi wakubwa kama Diamond na mara nyingi huambatana naye kwenye ziara zake za kimuziki ndani ya nchi.

MAI ZUMO

Anaingia kwenye listi hii japo ni mdogo kiumri akiwa na miaka minne tu, lakini maajabu yake sasa lazima ucheke.

Mai Zumo katika vipande vya video zake za kuchekesha, amekuwa akipewa sapoti kubwa na wazazi wake ambapo amekuwa akiwatumia katika kutengeneza vichekesho vyake.

KATARINA KARATU

Wengi wanamuita mdada wa Arusha kupitia lafudhi anayotumia ya Kimbulu, lakini ameweza kuwateka watu vilivyo kupitia Mtandao wa Instagram na mpaka sasa ameshatengeza jina lake vilivyo na kazi hiyo inampatia pesa kutokana na matangazo anayoyafanya.

KIPUPWE

Mchekeshaji huyu ametokea kujizolea umaarufu kupitia video fupifupi akiwa na Tin White na Ringo.

Kama umebahatika kuangalia filamu zake ikiwemo ya Pikipiki utaelewa jamaa anajua kuchekesha kwa kiasi gani.

MR BENEFICIAL

Jina lake halisi ni Bryan Anael. Ni mmoja wa vijana waliotengenezwa kwenye Kundi la Timamu.

Kupitia stand-up comedy, Beneficial amekuwa akifanya vichekesho vya majukwaani na kutengeneza vipande vya video kisha kutupia mtandaoni ambapo kwa sasa ni kama ameishika mitandao na lafudhi na staili yake ya ‘Machalii wa Arusha’.

MC PILIPILI

Wakati wasanii wa muziki wakiingiza mkwanja mrefu kwa shoo zao, huyu jamaa aliyekuwa mwalimu akaacha fani hiyo amekuwa akijaza kumbi mikoani kisha kuwachekesha na kujipatia jina kubwa na sasa analamba tu dili za ushereheshaji kwenye sherehe za harusi.

MAKALA: Imelda Mtema, DAR

‘KONKI MASTER’ ya Dudu Baya Yatikisa Morogoro!

Comments are closed.