The House of Favourite Newspapers

Wasanii wawapigia chapuo Dk. Magufuli, Idd Azan!

0

Mwandishi wetu

Lala salama! Wakati siku za kampeni zikiwa zimebaki 13, umoja wa wasanii wa tasnia mbalimbali wilayani Kinondoni, Dar umefanya tamasha maalum la kuwapigia chepuo na kuwaombea kura za ushindi wagombea wawili wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli kwa ngazi ya urais na Idd Azan kwa nafasi ya ubunge Jimbo la Kinondoni.

Katika tamasha hilo lililofanyika ndani ya Ukumbi wa Vijana Social uliopo Kinondoni, Dar, wasanii hao wa kada mbalimbali ikiwemo filamu, maigizo, ngoma za asili, muziki na uchoraji walisema kuwa ndani ya Ilani ya CCM kuna kipengele kinachoeleza namna ambavyo maslahi ya wasanii yataboreshwa hivyo wanaamini chama hicho kimewakumbuka na kwamba mafanikio kupitia sanaa yamewadia.

Walisema kingine kilichosababisha kuiamini ilani hiyo ni historia ya kiutendaji iliyotukuka ya mgombea urais wa chama hicho, Dk. Magufuli, hivyo wanaamini kilichoandikwa kitafanyiwa kazi pamoja na imani juu ya ufuatiliaji wa mambo wa Mbunge wa Kinondoni, Idd Azan anayetetea nafasi yake hiyo kwa mara nyingine.

Kwa niaba ya wasanii hao, mmoja wa waratibu wa tamasha hilo, Mkurugenzi wa Bendi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’, Asha Baraka alisema kuwa, kila kitu kipo wazi juu ya utendaji wa Magufuli kwani kila wizara aliyoitumikia ameacha alama nzuri na kazi zake zinaonekana kwa taifa huku akimsifia Idd Azan kwa staili yake ya kutekeleza ahadi zake bila mbwembwe na majigambo mengi.

“Sisi kama wa sanii wa kada mbalimbali, kama mnavyoona hapa kuna waigizaji, wanamuziki na kila aina ya wasanii, tumeamini kilichoandikwa katika ilani ya uchaguzi ya CCM, kinachotuaminisha ni histori ya utendaji wa Magufuli na ufuatiliaji wa mambo wa Idd Azan hivyo kila kilichoandikwa kuhusu uboreshwaji wa masuala yote ya sanaa, tunaamini kitafanyika, tunakiombea kura za ushindi Chama Cha Mapinduzi,” alisema Asha Baraka kwa niaba ya wasanii hao.

Leave A Reply