Washindi wa Shindano la Startupper of The Year Watangazwa
TotalEnergies Tanzania inayo furaha kutangaza washindi watatu wa Shindano la ‘Startupper of the Year’ kwa mwaka 2024. Shindano hili, lililowazi kwa wajasiriamali vijana wa Kitanzania wenye umri wa miaka 18 hadi 35, linatoa nafasi ya kuangazia mawazo bunifu ya kibiashara na kuanzisha biashara zenye maono ya baadaye kote nchini.
Shindano la Startupper of the Year 2024 lilianza Aprili 30, likiwavutia wajasiriamali vijana kutoka nchi 32 za Afrika, na washindi 100 wakichaguliwa na majopo wa ndani na kutoka nje. Toleo la mwaka huu, ambalo ni sehemu ya kusherehekea miaka mia moja ya TotalEnergies, liliwatunuku washindi wa Kitanzania katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika ofisi za TotalEnergies jijini Dar es Salaam.
Washindi wa ndani ya nchi ni Bi. Editha Godlisten, aliyeshinda Tuzo ya Mjasiriamali Bora kwa mradi wake, Freshpack Technologies, Bi. Adelaide Mwasyoghe, ambaye mradi wake, Sustainable Avocable Oil, umeshinda Tuzo ya Mradi Bora wa Uchumi; na Bi. Emman Mohamed, aliyepata Tuzo ya Mradi Bora Endelevu na Nafuu kwa mradi wake wa Non-Refillable Oxyvent.
Kila mshindi atapokea ufadhili wa TZS milioni 20, fursa za kuonekana kwenye vyombo vya habari vya ndani na majukwaa ya kidijitali ya TotalEnergies, na mafunzo binafsi kutoka kwa Westerwelle Foundation Tanzania ili kuwasaidia kukuza na kupanua miradi yao.
Mamadou Ngom, Mkurugenzi Mtendaji wa TotalEnergies Tanzania, alisisitiza dhamira ya kampuni hiyo ya kuwaunga mkono wajasiriamali vijana: “Kuwaunga mkono vijana wenye vipaji ni muhimu kwa mustakabali wa bara letu. Kupitia programu hii, TotalEnergies inatarajia kuimarisha uchumi wa ndani, kuhamasisha ari ya ujasiriamali, na kukuza miradi inayojali jamii na mazingira.”
Mmoja wa washindi, Bi. Emman Mohamed, anayeongoza mradi wa ugavi wa oksijeni kwa hospitali, alishukuru kwa kutunukiwa, akisema, “Tuzo hii inanipa motisha ya kuendeleza mradi wangu ambao unaleta rasilimali muhimu kwa vituo vya afya.”
Kwa zaidi ya maombi 1,000 na jumla ya maombi 436 yaliyowasilishwa kutoka Tanzania, shindano hili lilimalizika kwa tukio la mwisho ambapo washiriki 15 bora walitoa mawasilisho yao mbele ya jopo la majaji. Ushiriki huu wa juu unaakisi hamasa na ubunifu wa vijana wa Kitanzania waliojitolea kutatua changamoto halisi za dunia.