Washukiwa wa bomu bandia ndege ya Air France wakamatwa Ufaransa
Abiria wa ndege hiyo wakiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kenya baada ya kuokolewa.
MAOFISA wa Polisi nchini Ufaransa wamewatia mbaroni abiria wawili wa ndege hiyo ambao ni mke na mme liokuwa abiria katika ndege ya Air France Boeing 777 nambari AF463 iliyolazimika kutua kwa dharura nchini Kenya hapo jana kufuatia tishio la bomu.
Duru zinasema kuwa wawili hao ambao majina yao bado hayawekwa hadharani walikamatwa punde baada ya kutua katika Uwanja wa Kimataifa wa Charles de Gaulle nchini Ufaransa.
Ndege ya shirika la Air France.
Waliokamatwa ni ofisa mmoja mstaafu wa polisi ambaye ni mshukiwa mkuu huku mkewe akishikilwa ili kutoa shahidi wa tukio hilo.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege la Air France alifutilia mbali tahadhari ya bomu iliyosababisha ndege hiyo ya kutua kwa dharura Kenya na kusema kuwa lilikuwa bomu bandia.
Abiria baada ya kuokolewa.
Frederic Gagey aliwaambia waandishi wa habari mjini Paris, Ufaransa kuwa kifaa kilichodhaniwa kuwa kilipuzi kilikuwa ni mbao na kisanduku cha karatasi tu wala hakikuwa na uwezo wowote wa kuhatarisha usalama wa ndege hiyo.
Abiria baada ya ndege hiyo kutua kwa dharura Kenya.
Inasemekana kuwa abiria mmoja alikipata kifaa hicho chooni na akamfahamisha mhudumu mmoja wa ndege hiyo.
Ndege hiyo ilikuwa na abiria 459 na wahudumu 14.
Bomu bandia lililokutwa kwenye ndege hiyo
Mhudumu huyo alimfahamisha rubani kuhusiana na kifaa hicho na shughuli za kutua kwa dharura zikaanza.
Ndege hiyo ilitua saa sita usiku wa kuamkia Jumapili, huku wataalamu wa kutegua mabomu kutoka jeshi la wanamaji la Kenya wakiingia ndani ya ndege hiyo kukagua kifurushi kilicholeta taharuki.
Sasa kitengo cha ujasusi cha Ufaransa kimeanzisha uchunguzi wa kina kubaini kilichosababisha tishio hilo.
PICHA NA DAILY MAIL