Wasiooga marufuku jijini Dar es Salaam – Makonda
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Paul Makonda, amepiga marufuku ‘watu wachafu’ kuonekana mitaa ya jiji hilo katika kipindi cha mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Mkutano huo wa 39 wa SADC unatarajiwa kufanyika mwezi ujao, Agosti 18 na 19 mwaka huu. Kama sehemu ya maandalizi ya mkutano huo, Makonda amesema jiji hilo leye wakazi wengi zaidi nchini Tanzania litakuwa katika hali ya usafi mkubwa.
Kwa mujibu wa shirika la utangazaji la Uingereza (BBC) amesema:
“Tabia ya kuja mjini bila kunyoosha nguo ni marufuku. Tabia ya kuja mjini hujaoga ni aibu. Watu wanatembea tu na chawa, kama huwezi kuwa msafi basi subiri mwezi huu upite,” Makonda amenukuliwa na gazeti la Mwananchi la nchini humo akisema na kuongeza: “Kwa kipindi hiki tuvumiliane, kama hufui nguo, kama huogi, pumzika kidogo kuja mjini.”
Sababu ya kutoa amri hiyo kwa mujibu wa Makonda ni kuepuka “kumtia aibu Rais wa Tanzania John Magufuli mbele ya marais kutoka nchi 15 watakaokuwa hapa nchini.” Pia, Makonda ameagiza kwamba mtu yoyote mwenye gari atakayetupa takataka barabarani asitozwe faini, badala yake apewe eneo la kufanya usafi. Amesema baadhi ya watu hao wana jeuri ya fedha, hivyo kwao faini siyo adhabu.
“Mtu mwenye gari akitupa takataka msimtoze faini, mshusheni kwenye gari, mpeni kipande cha kilomita moja cha barabara apige deki. Hawa watu fedha kwao siyo tatizo, sasa tunataka kuwaonyesha kwamba na sisi tuko ‘serious’ na usafi wa jiji letu.”
CHANZO: BBC SWAHILI
Comments are closed.