The House of Favourite Newspapers

Watano Wafa Shambulio la Kigaidi Yemen Serikali Mpya Ikianzishwa

WATU wasiopungua watano wameuawa na makumi kadhaa kujeruhiwa katika shambulio lililofanywa katika uwanja wa ndege wa mjini Aden, Yemen, muda mfupi baada ya ndege iliyokuwa na viongozi wa serikali mpya ya Yemen ilipowasili kutoka Saudi Arabia.

 

Shambulio hilo lilifanywa wakati maofisa wa serikali hiyo walipokuwa wakishuka katika ndege, ambapo milipuko mikubwa na risasi vilinaswa katika kamera uwanjani hapo ambapo watu waliokuwa karibu — waandishi wa habari na maofisa usalama — walibidi kukimbia kutoka eneo hilo.

 

Mawaziri watarajiwa, akiwemo Waziri Mkuu, Maeen Abdulmalik, na Balozi wa Saudi Arabia nchini Yemen, Mohammd Said al-jaber, walikimbizwa na kupelekwa katika Ikulu ya Rais ya Mashiq.

Pamoja na tukio hilo, hakuna mtu miongoni mwa maofisa wa serikali hiyo  aliyedhurika.  Waziri wa Mawasiliano wa Yemen, Naguib al-Awg, aliyekuwa katika ndege hiyo ya serikali, alisema alisikia milipuko miwili iliyoashiriia kwamba zilikuwa ni ndege zisizokuwa na rubani.

 

“Ingekuwa balaa iwapo ndege ingeshambuliwa kwa bomu,” alisema akisisitiza kwamba ndege hiyo ilikuwa lengo la shambulio hilo.

 

Chanzo cha milipuko hiyo hakikufahamika vizuri, lakini vyombo vya usalama katika eneo hilo  vilisema mabomu yalianguka katika ukumbi wa mapokezi wa uwanja huo.

 

Serikali ya Rais Hadi na wapiganaji wanaotaka kujitenga kusini mwa nchi hiyo, wanaendesha mapigano dhidi ya waasi wa Houthi.