Watanzania Wahimizwa Kuchukua Hatua za Kuzuia Magonjwa ya Zuonotiki
Serikali ya Tanzania, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ikishirikiana na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) kupitia mradi wa Breakthrough ACTION, wameungana na mataifa mengine katika kuadhimisha Siku ya Magonjwa ya Zuonotiki Duniani, ikitumia fursa hii kuwahamasisha Watanzania kuhusu magonjwa ya zuonotiki, yaani magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu na kuhimiza juhudi za pamoja za kuzuia na kudhibiti magonjwa haya.
Siku ya Magonjwa ya Zuonotiki Duniani ilianza kuadhimishwa kwa heshima ya kazi ya Mwanasayansi Louis Pasteur, ambaye alifanikiwa kutoa chanjo ya kwanza dhidi ya kichaa cha mbwa mnamo Julai 6, 1885.
Maadhimisho haya ya kila mwaka yanatukumbusha kwamba magonjwa ya zuonotiki yanaendelea kuwa changamoto kubwa ya afya ya umma, huku takwimu za hivi karibuni zikionyesha kuwa asilimia 60 ya magonjwa yote yanayosababisha milipuko yanatoka kwa wanyama.
“Tunawahimiza Watanzania kuchukua jukumu la kulinda afya zao kwa kuzingatia usafi binafsi, kupata matibabu mara wanapohisi wameambukizwa ugonjwa wa zuonotiki, na kuripoti vifo vya ghafla vya wanyama kwa wataalam wa mifugo ndani ya jamii zao,” alisema Dk. Salum Manyatta, Mkurugenzi Msaidizi- Sehemu ya Afya Moja katika Ofisi ya Waziri Mkuu.
Tanzania imeyapa kipaumbele magonjwa sita ya zuonotiki kutokana na athari zake kubwa kwa jamii: kichaa cha mbwa, kimeta, brusela, mafua ya ndege, malale na homa ya kuvuja damu kama Marburg na Ebola,
Wataalamu wanasisitiza kutumia mbinu ya Afya Moja katika kupambana na kuzuia magonjwa haya kwa ufanisi. “Kichaa cha mbwa ni tatizo kubwa kutokana na kiwango chake cha juu cha vifo na maambukizi mengi kwa watoto,” alisema Dk. Manyatta.
Magonjwa ya zuonotiki yanaweza kuambukizwa kupitia njia mbalimbali, ikiwemo kugusana moja kwa moja na wanyama walioambukizwa, kula chakula kisichoiva vizuri hasa nyama na maziwa, kuvuta hewa yenye chembechembe za vimelea vya magonjwa, kung’atwa au kukwaruzwa na wanyama wenye maambukizi.
“Kula nyama isiyopikwa vizuri na kuzika myama aliekufa bila usimamizi inaweza kusababisha maambukizi ya magonjwa kama kimeta,” alisisitiza Dk. Stanford Ndibalema, Mkurugenzi Msaidizi Afya ya Jamii kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Ili kupambana na magonjwa haya, Serikali imezindua kampeni ya kitaifa iitwayo “Holela Holela Itakukosti” ili kuwezesha majadiliano kuhusu magonjwa ya zuonotiki na kuhimiza jamii kuchukua hatua sahihi kupambana na magonjwa haya.
Kampeni hii inalenga kuwahamasisha watanzania kuchukua jukumu la kutunza afya zao kwa kuzingatia usafi binafsi, kwenda mara moja kwenye kituo cha afya pale wanapohisi wameambukizwa ugonjwa wa zuonotiki, na kuripoti vifo vya ghafla vya wanyama kwa wataalam wa mifugo ndani ya jamii zao.
“Kampeni hii ni muhimu katika kuongeza uelewa kuhusu magonjwa ya zuonotiki na kusaidia jamii kuchukua hatua sahihi ili kupambana na magonjwa haya,” alisema Dk. Manyatta na kuongeza: “Kwa kufanya kazi pamoja, tunaweza kuzuia magonjwa haya yasisambae na kuhakikisha Tanzania yenye afya bora.”
Jamii inahimizwa kuchukua hatua chanya za kuzuia na kutibu kama vile kuchanja wanyama, kupika chakula vizuri, na kushughulikia wanyama waliokufa kwa usahihi. “Tumekuwa tukiwasihi watu kuripoti vifo vyovyote vya ghafla vya wanyama kwa wataalam wa mifugo ndani ya jamii zao,” alisema Dk. Ndibalema.