The House of Favourite Newspapers

Watanzania wamechoka, CCM, Ukawa msiwachukulie poa!

0

magufuli akifanya mkutano wake wa mwisho mjini kahama leo katika viwanja vya UWT CCM KahamaKUNA maneno mengi katika majukwaa ya wanasiasa kwa sasa, nchi ikijiandaa kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika wiki ya mwisho ya mwezi huu. Kama ambavyo tumekuwa tukisema mara zote, safari hii hali ni mbaya mno kwani upinzani ni wa hali ya juu.

Katika majukwaa, kuna mashambulizi makali kwa kila upande, wote wakijinasibu kuwa wao ndiyo hasa wenyewe katika kutafuta muarobaini wa matatizo yanayowakabili Watanzania.

Ni kweli, Watanzania kwa ujumla wao, wana hali ngumu sana. Maisha ni magumu kila upande, kitu pekee walicho na uhakika nacho, ni pumzi maana wanaipata bure na hakuna mizengwe!

lowassaaKuna watu, wale wenye neema zilizotokana na ubinafsi wao katika kuila keki ya taifa, hawaamini kama leo hii Watanzania wanaweza kusema hapana sehemu ambayo wao waliwazoesha kusema ndiyo. Wanaposikia neno hapana, akili zao zinawatuma kuamini kuwa maneno hayo yamepandikizwa.

Inakuwa vigumu kwa mfano, mtu wa CCM kuamini kuwa mamia kwa maelfu ya watu wanaweza kukusanyika katika eneo linalohutubiwa na mwanasiasa wa upinzani, kisha wakampigia makofi. Akilini mwa mtu huyu wa chama tawala, kuna imani kwamba watu hao wametengenezwa kwa lengo la kuonesha kuwa hawakubaliki.

Siwezi kusimamia sana katika hili kwa sababu kwenye siasa, hasa hizi za Bongo, kila jambo linawezekana. Ninachotaka kuamini, hata kama adhabu yake itakuwa ni umauti, ni kwamba wapo Watanzania, tena wengi tu, wanaotaka mabadiliko!

Hawa hawasukumwi na fedha za mtu wala umaarufu wake, isipokuwa wamechoka aina ya maisha wanayoishi sasa.

Wametengwa, nchi ya wote lakini imegeuka kuwa ya watu wachache na kutufanya wote tuliobaki kuwa wapambe.

Ni nchi nzuri kwa familia za viongozi na wafanyabiashara wakubwa.

Wao wanapata kila kitu, tuliobaki tunakosa vitu vyote na vile vidogo tunavyobahatisha, tunakatwa kodi.

Kwa nini ninasema hivi, ni kwa sababu ninataka kuwakumbusha chama tawala kuwa hawana sababu ya kuwaona watu wanaoshabikia upinzani kama wajinga au walionunuliwa, isipokuwa hili ni zao lililozalishwa na CCM, likapaliliwa na sasa limestawi.

Hawana sababu ya kumshambulia Edward Lowassa kwa maneno ya kebehi wala kejeli, kwa sababu huyu mtu hana uwezo wa kuwaambia watu kitu wasichokitaka. Inawezekana kabisa kuwa mbunge huyu wa Monduli ni fisadi, ana mapesa mengi na utajiri wa kutisha, hivyo anakosa sifa za kuwa rais wetu, lakini je, tuwaache CCM waendelee kufanya kama wanavyofanya kwa sababu tu mgombea wetu hana sifa?

Kuna kitu kimoja cha dhahiri ambacho CCM wanapaswa kukifanya endapo watashinda. Nacho ni kubadili mtazamo wao wa kifikra na kuamini kuwa Watanzania wa sasa wamechoshwa, siyo na CCM kama chama, bali na jinsi wanavyoishi kinyonge katika nchi yao tajiri.

Unapowachosha watu kwa staili hii, ni hatari kwa sababu mwisho wa siku wataamua tu kukikataa chama bila kujali ni nani anawasimamia. Watu wangeweza kuifanya ajenda hoja ya kutokuwa na maadili kwa Lowassa kama kungekuwa na maadili ndani ya chama.

Sasa leo unatuambia huyu fisadi bila kutuonesha muadilifu?

Ili kujenga uhalali, ni lazima chama hiki kifanye mageuzi ya kweli, ili hawa vijana ambao leo wanasema wamekunywa viroba wasionekane mtaani, vinginevyo, wakati ujao watakuwa nje ya mageti ya wakubwa wakiwasubiri wagawane walichonacho!

Leave A Reply