The House of Favourite Newspapers

Watanzania watatu walamba dume FC Barcelona

0

Sweetbert Lukonge, Dar es Salaam

WAKATI Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likiwa katika harakati za kuhakikisha mchezo wa soka unapiga hatua, makocha watatu kutoka hapa nchini wamelamba dume baada ya kuchaguliwa kwenda kupata mafunzo ya ukocha kutoka FC Barcelona.

Mafunzo hayo yanafanyika Lusaka nchini Zambia na yanaendeshwa na makocha mahiri kutoka FC Barcelona ambayo ni moja kati ya timu za kiwango cha juu kabisa katika mchezo wa soka hapa duniani.

Meneja wa Bia ya Castle hapa nchini ambao ndiyo wadhamini wakuu wa mafunzo hayo, Kabula Nshimo, ameliambia gazeti hili kuwa, makocha waliopata bahati hiyo ya kuiwakilisha Tanzania katika mafunzo hayo ni Maalim Salehe Mohamed, Kessy Claud Mziray na Shaweji Ismail Nawanda.

“Tunayo furaha kubwa kuwapeleka makocha hawa watatu na tuna matumaini kuwa watapata uzoefu mkubwa kutoka kwa makocha hao wa FC Barcelona ambao tayari wapo nchini Zambia ili kusaidia kunyanyua kiwango cha soka barani Afrika,” alisema.

Katika hatua nyingine, Rais wa TFF, Jamal Malinzi, ameipongeza Bia ya Castle kwa juhudi hizo endelevu kwa kusema kuwa makocha hao watatu waliochaguliwa wapo katika programu za maendeleo za shirikisho hilo, hivyo ni matumaini yake kuwa watapata mambo mengine muhimu kwa ajili ya faida ya soka la Tanzania.

Leave A Reply