The House of Favourite Newspapers

Watanzania Wang’ara Marekani, Wajishindia Mil 168 Ubunifu wa Miradi

0
Washiriki wote waliofikia fainali za shindano lililoendeshwa na taasisi ya Conscious Capitalism wakiwa jukwaani ambapo Benjamin (kulia) akifuatiwa na Bernice walishiriki.
Benjamin akielezea furaha yake mwishoni mwa shindano hilo.
Bernice akitoa neno la shukurani kwenye hafla hiyo.

WATANZANIA wawili wwenye Shahada ya Uzamili ya Uongozi katika Biashara (MBA), wameshika nafasi ya kwanza na kutunukiwa Dola 75,000 (sawa na Sh. milioni 168 za Tanzania) kwenye shindano la ubunifu wa miradi mbali ya kibiashara inayoandikwa na kupendekezwa na wahitimu wa vyuo vikuu ambayo yalihitimishwa hivi karibuni katika  Jimbo la Pennysylvania, Marekani.

Bernice na Benjamin Fernandes ni dada na kaka kutoka Tanzania waliokuwa wakisoma nchini Marekani.

Bernice Fernandes  ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Pepperdine kwa shahada mbili za uzamivu kwa daraja ya juu (honors), wakati kaka yake Benjamin Fernandes ni mhitimu wa Shahada ya Uzamili ya Uongozi katika Biashara (MBA) kutoka chuo cha Stanford Graduate School of Business.

Benjamin na Bernice walibuni miradi mbalimbali ya  kijamii wenye lengo la kuingiza faida nchini Tanzania, na walituma maombi ya kushiriki katika mashindano  hayo ya vyuo vikuu kuhusiana na masuala ya miradi ya biashara yaliyofanyika nchini Marekani.

Mashindano hayo hufanywa na taasisi ya Conscious Capitalism.   Hii ni taasisi inayoamini katika biashara ya soko huria (ubepari) ukiwa ndiyo mfumo wenye nguvu zaidi kiuchumi katika ushirikiano wa kijamii na ustawi wa binadamu, kama ukitumika ipasavyo

Conscious Capitalism  huanzisha biashara mbalimbali zenye ubora wa hali ya juu na zenye kufuata maadili yanayotakiwa.  Taasisi hii huyasaidia makampuni mbalimbali kwenda sambamba na mabadiliko mbalimbali ambayo yanachochea juhudi zaidi, kupanua elimu na kuwezesha kumwendeleza binadamu kupitia biashara.

Mashindano hayo ya ubunifu wa mipango ya biashara yalifanyika  kati ya Aprili 18 hadi 20.  Miongoni mwa maombi mengi yaliyopokelewa kutoka kwa washiriki wa mabara matatu duniani,  timu yao ilichaguliwa kuendelea katika Fainali za Kitaifa wakiwa moja ya timu nne za juu kufikia fainali.

Bernice na Benjamin walishindanisha ubunifu wao  dhidi ya miradi mitatu iliyokuwa na wahitimu kutoka Chuo Kikuu cha Drexel University, Chuo Kikuu cha Kentucky  na Akademia ya Maji ya Marekani (United States Naval Academy).
Bernice na Benjamin waliwasilisha mradi wao kwa bashasha kubwa, utaalam wa hali ya juu, mikakati kabambe na ujuzi wa kuhudumia mradi huo.  Baada ya kuhojiwa kuhusu miradi yao na kufanyika majadiliano makubwa kati yao na  majaji husika,  walitunukiwa zawadi ya kwanza ya Dola75,000 ambazo ni sawa na Sh. milioni 168 za Tanzania.

Katika kupokea zawadi hiyo, Bernice alisema: “Hatukushinda kama timu tu, bali tumeipa nchi yetu ya Tanzania ushindi.  Hii ni dhamira yangu ya kuendeleza biashara nchini Tanzania kwa ajili ya Watanzania na kupitia Watanzania.”

Leave A Reply