Watatu Kortini Kwa Kudaiwa Kuiba Madini

WATU watatu wakazi wa Jijini Dar es Salaam wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi likiwemo shtaka la kuiba madini  yenye thamani ya Sh 507,347,000.

Wakisomewa  hati ya mashtaka, na wakili wa Serikali, Jacqueline Nyantori amewataja washtakiwa hao kuwa ni, Donald Njonjo (30) Mkazi wa Kigamboni, Gamba Muyemba (51) Mkazi wa Tandika na Kashif Mohamed (41) Mkazi wa Upanga jijini Dar es Salaam.

Watuhumiwa hao wamesomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mwandamizi Mfawidhi, Kelvin Mhina ambapo imedaiwa kuwa kati ya Novemba 30, 2017 na Juni 29, mwaka huu katika Ofisi ya Tume ya Madini iliyopo Masaki wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaam washtakiwa hao waliba madini ya dhahabu yenye uzito wa Kilogramu 6.244 yenye thamani ya Sh 507,347,000 mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Inadaiwa kuwa, Julai 8, mwaka huu katika mtaa wa Indiragandhi wilayani Ilala jijini Dar es Salaam mshtakiwa Mohamed alikutwa na madini ya dhahabu yenye uzito wa gramu 2794.5 ya Dola za Marekani 121,155.45 sawa na Sh 278,714,478.06 mali ambayo imeibiwa kwenye Tume ya Madini.

Katika shtaka la tatu imedaiwa kati ya Julai Mosi, 2018 na Novemba 31, mwaka jana katika maeneo mbalimbali  wilaya ya Ilala, washitakiwa kwa pamoja waliuza madini ya dhahabu yenye uzito wa Kilogramu 6.244 ya thamani ya Sh 507,347,000 bila kuwa na kibali.

Pia inadaiwa, kati ya Julai Mosi, 2018 na Novemba 31, 2018 katika maeneo mbalimbali washtakiwa hao walijihusisha moja kwa moja na muamala unaohusu madini hayo ya dhahabu wakati wakijua kuwa dhahabu hiyo imetokana  na kosa tangulizi la wizi.

Hata hivyo, washitakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 29, mwaka huu ambapo  itatajwa na washitakiwa wamerudishwa rumande.


Loading...

Toa comment