WATU watatu wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka matano ikiwemo kosa la uhujumu uchumi na utakatishaji waDola za Marekani zaidi ya 300,000 mali ya Kampuni ya SMCI ya Marekani.
Washitakiwa hao Deogratias Masika, William Kimonge, wakazi wa Dar es Salaam na Youssouf Sabo raia wa Cameroon wamesomewa shitaka lao mbele ya Hakimu mwandamizi wa mahakama hiyo Cassian Matembele.
Wakili wa Serikali Annastazia Wilson, amedai kuwa washitakiwa hao kati ya Desemba 2016 na Januari 2017 jijini humo, walilaghai Kampuni ya SMCI ya Marekani na kujipatia dola za Marekani 300,020 na ishirini wakidanganya kuwa wataisambazia kampuni hiyo tani elfu tano za korosho kutoka Mtwara wakati haikuwa kweli.
Katika shitaka la tatu na la nne ambalo ni la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, washitakiwa hao wanadaiwa kuilaghai kampuni hiyo nakujipatia Dola 15,000 za Marekani wakidanganya kuwa wataisambazia kampuni hiyo tani elfu kumi za korosho kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam wakati haikuwa kweli.
Aidha washitakiwa hao wanadaiwa kuilaghai kampuni hiyo na kujipatia Dola za Marekani zaidi ya laki tatu na kuzingiza kwenye Account ya CRDB yenye jina la JAW Distributors Limited kwa lengo la kubadilisha kuwa fedha za Kitanzania.
Hata hivyo, washitakiwa hao wamekana shitaka linalowakabili huku hakimu anayeendesha shauri hilo akidai dhamana ipo wazi kwa mshitakiwa namba mbili ambaye ametakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya milioni sitini na tisa kila mmoja.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septamba 29 mwaka huu na washitakiwa wote wamerudishwa mahabusu.